Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mabalozi,Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa yaliyopo hapa Nchini kwa lengo la kuwapa mrejesho kuhusu Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.

Akizungumza na Mbalozi,Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa Balozi Mulamula amesema Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano uliofanyika Lilongwe Malawi 17 -18,Agosti,2021 kwa pamoja walikubaliana kuendelea kukabiliana na janga la UVIKO -19 ikiwa ni pamoja na kushawishi Kampuni zinazozalisha chanjo kutoa kibali ili teknolojia yao itumike kuzalisha chanjo hizo katika Nchi zinazoendelea kurahisha upatikanaji wa chanjo hiyo kwa wote na kwa bei nafuu.

Pia amewaeleza Mabalozi,Wakuu wa Taasisi na Mashirika  kuhusu ombi la Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuzisihi Taasisi za fedha za Kimataifa pamoja na Nchi zilizoendelea kutoa msamaha au kurefusha muda wa urejeshwaji wa mikopo hadi pale janga hili la UVIKO 19 litakapopatiwa ufumbuzi.

Kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mpango wa SADC wa kupeleka Jeshi katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji Balozi Mulamula amesema suala la ulinzi na usalama kwa nchi za SADC ni ulinzi na usalama kwa Tanzania,hivyo Tanzania imeshiriki kikamilifu kwa kutoa mchango wake wa fedha pamoja na jeshi.

Pia Balozi Mulamula ametoa msisitizo kwa Mabalozi wanaokwenda Mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Bw. Freeman Mbowe kufuata sheria na taratibu za Kimataifa kuhusu masuala ya Kidiplomasia ili kujiepusha na ukiukwaji wa sheria na taratibu hizo.

Balozi Mulamula amefafanua kuwa Serikali haina lengo la kuwazuia Mabalozi hao kwenda mahakamani kufuatilia kesi hiyo,lakini kutokana na na uwepo wa janga la UVIKO -19 pamoja na msongamano ni muhimu kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na  kufuatilia shauri hilo kwa njia nyingine ikiwemo kupitia vyombo vya habari.

Amesisitiza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndio yenye jukumu la kuhakikisha usalama wa Wanadiplomasia waliopo hapa nchini. Hata hivyo,kwa siku za hivi karibuni baadhi ya Wanadiploamasia hao wameonekana mahakamani bila kufuata sheria,kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya Kidiplomasia ikiwemo kutoa taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kiongozi wa Mabalozi waliopo hapa Nchini Dkt. Ahamada El Badaoui amesema ulinzi wa Mabalozi waliopo hapa Nchini ni muhimu sana na kuongeza kuwa endapo kuna mabalozi wanafanya hivyo ni vyema wakafuata taratibu na sharia zilizopo jambo lililoungwa mkono na Balozi wa Zambia hapa Nchini Mhe. Benson Keith Chali.

Katika Mkutano huo baadhi ya Mabalozi wamepongeza mafanikio yaliyopatikana na kueleza kuridhishwa na namna Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inavyoendesha shughuli zake pamoja na namna inavyotatua changamoto mbalimbali.