Wanamgambo wa itikadi kali wa Taliban wameimarisha udhibiti wao kwenye maeneo waliyoyakamata nchini Afghanistan, ambapo sasa wanadhibiti asilimia 65 ya nchi. 

Pul-e-Khumri, mji mkuu wa mkoa wa kaskazini wa Baghlan uliangukia mikononi mwa Taliban jana jioni na kuwa mji mkuu wa saba wa kikanda kukamatwa na wapiganaji hao katika wiki moja. 

Rais wa Marekani Joe Biden amewahimiza viongozi wa nchi hiyo kuipigania nchi yao. Biden amewaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kuwa viongozi wa Afghanistan wanapaswa kuungana, akiongeza kuwa wanajeshi wa Afghanistan ni wengi kuliko Wataliban na lazima wapambane. 

Rais huyo wa Marekani amesema hajutii uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi wake Afghanistan, akidokeza kuwa Marekani imetumia zaidi ya dola trilioni moja kwa zaidi ya miaka 20 na kuwapoteza maelfu ya wanajeshi. Amesema Marekani itaendelea kutoa msaada wa angani, chakula, vifaa na mishahara kwa wanajeshi wa Afghanistan.