Rais Joe Biden wa Marekani amesema ameidhinisha vikosi zaidi vya Wanajeshi wa Marekani viende katika mji Mkuu wa Afghanistan, Kabul, kusaidia ulinzi wa ubalozi wa Marekani na kuwaondoa Wafanyakazi wake kutoka Taifa hilo linaloelekea kuangukia mikononi mwa Wanamgambo wa Taliban.

Biden amesema kutokana na ushauri wa Wataalamu wa diplomasia, Jeshi na Ujasusi ametoa idhini ya kutumwa Wanajeshi 5,000 kuhakikisha usalama wa Wamarekani na Washirika wao unakuwepo.

Katika tamko refu lililotolewa jioni ya jana, Biden ametetea uamuzi wake wa kuwaondoa Wanajeshi wa Marekani Afghanistan baada ya miaka 20 ya kuwepo kwao Nchini humo.

Biden amesema Marekani iliwaambia Wanamgambo wa Taliban kwenye mazungumzo ya Qatar kwamba kitendo chochote kitakachohatarisha maisha ya Wamarekani nchini Afghanistan kitajibiwa kwa hatua kali ya kijeshi.