Rais wa Tanzania, Samia Suluhu anatarajia kuondoka nchini Jumanne Agosti 24, 2021 kuelekea nchini Zambia kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zambia, Hakainde Hichilema.

Sherehe za kumuapisha Hichilema ambaye ni Rais wa saba wa Zambia zitafanyika katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium) jijini Lusaka.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Agosti 23, 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu imeeleza kuwa katika msafara wake Rais Samia ataongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni wa CCM, Maudline Cyrus Castico.

Wengine ni Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mizengo Peter Pinda, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kombo Hassan Juma, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Henry Shekifu, na Mbunge wa Jimbo la Mtera na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Livingstone Lusinde.
Advertisement

Vilevile, taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete atashiriki katika sherehe hizo akiwa kiongozi wa timu ya waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Madola.