Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Watu watatu wameuawa kikatili katika matukio mbalimbali yaliyotokea mkoani Pwani ,ikiwa ni pamoja na mwanamke kubakwa hadi kifo na mwanamke mwingine kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kutenganishwa na kiwiliwili.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,Wankyo Nyigesa alisema tukio la kwanza lilitokea Agosti 8, mwaka huu katika Kitongoji cha Tobora Kata ya Msata ambapo mwanamke mmoja (26) Mzigua ,Mkazi wa Pongwe Msungura alibakwa kisha kuuawa .


Mwanamke huyu mwili wake ulitelekezwa vichakani, mtuhumiwa mmoja amekamatwa kuhusiana na tukio hilo na Jeshi la Polisi linaendelea kumhoji.


Katika tukio jingine Kamanda Nyigesa,alisema mwanamke mwingine ambaye jina lake limehifadhiwa Mkazi wa Kijiji cha Kitonga Wilayani Bagamoyo aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni kisha kutenganisha kichwa na kiwiliwili.


Nyigesa,alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 4 mwaka huu saa 12 jioni huko katika Kijiji cha Kitonga ambapo marehemu alivamiwa shambani kwake na watu wasiojulikana na hivyo kutekeleza mauaji hayo.


Pamoja na hayo ,mtu mmoja mkazi wa Kijiji cha Kwarohombo Kata ya Mbwewe Chalinze ambaye jina lake halijafahamika aliuawa kwa kupigwa mkuki na wafugaji ambapo hata hivyo Jeshi la Polisi lipo katika msako dhidi ya wahalifu hao.


Wakati huo huo ,Jeshi hilo linamshikilia Sijali Idd akiwa na Gobole moja ,unga wa baruti na gololi 11zinazotumika katika Gobole hilo.


Kamanda Nyigesa,alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 4 mwaka huu saa 11 jioni katika Kijiji cha Msimbani Kata ya Miono Wilayani Bagamoyo.


Alibainisha mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia silaha hiyo kufanya shughuli za uwindaji kinyume na utaratibu lakini atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.


Katika hatua nyingine,Nyigesa alitoa wito kwa wananchi kutii sheria bila shuruti na kutoa taarifa za kiuhalifu kwa Jeshi hilo na vyombo vingine vya dola ili wahalifu hao wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo.