Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesema kupata chanjo ya virusi vya corona ni kitendo cha upendo na amewataka watu kuchanjwa. 

Katika ujumbe wake uliotolewa leo kwa njia ya video, Papa Francis amesema anamshukuru Mungu kwa Neema zake na kazi kubwa iliyofanywa na watu, chanjo ya kuwalinda na COVID-19 imepatikana. 

Amesema chanjo hiyo inatoa matumaini ya kuondokana na janga hilo, lakini iwapo tu zitawafikia watu wote na ikiwa watu watafanya kazi kwa pamoja. 

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani amesema kuchanjwa ni njia rahisi, lakini yenye faida kwa wote na kuhakikisha usalama wa kila mtu, hasa walioko hatarini. 

Video hiyo imetolewa kwa lugha ya Kihispania kama sehemu ya kampeni ya kimataifa inayoitwa ''Inategemea wewe'' yenye lengo la kuhamasisha chanjo dhidi ya virusi vya corona.