Na Mwandishi Wetu, Tunduru
Serikali imesema haitofumbia macho Shirika lolote Lisilo la Kiserikali litakalofanya kazi kinyume na Katiba zao na dhumuni la Shirika husika.

Agizo hilo limetolewa na  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma kukagua shughuli mbalimbali za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Wilayani humo.

Naibu Waziri Mwanaidi amesisitiza kuwa lengo la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni kusaidia pale ambapo Serikali haijafika katika kutoa huduma kwa jamii na sio vinginevyo.

"NGOs hizi zinasajiliwa kwa mujibu wa Sheria sasa niziombe tu zifanye kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo hatutofumbia macho ukiukwaji wowote wa Sheria na taratibu" alisema Mhe. Mwanaidi

Aidha ameongeza kuwa zipo changamoto nyingi katika jamii ikiwepo vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikikatisha ndoto za watoto wa kike walio wengi katika meneno mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mhe. Dkt. Julius Kenneth Ningu amesema watahakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi katika Wilaya ya Tunduru na Mkoa kwa ujumla yanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.

"Tutahakikisha NGOs zinafuata Sheria na zinafanya kazi kwa mujibu wa usajili wao na kuwanufaisha wananchi" alisema Dkt. Ningu

Ameongeza kuwa Wilaya itasimama vizuri katika kuhakikisha inawachukulia hatua wanaosababisha kuwepo kwa mimba za utotoni

Akizungumza Mratibu wa Mradi wa Afya Mama na Mtoto Katibu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Masasi Phares Lihewe amesema mradi huo umechangia katika kutoa elimu na vifaa vya kunawa mikono ikiwa ni hatua za kujikinga na UVIKO 19 katika Shule mbalimbali za Sekondari Wilayni Tunduru.

Katika ziara yake Wilayani Tunduru Naibu Waziri Mwanaidi amekabidhi vifaa vya kunawa mikono kwa baadhi ya Shule za Sekondari Wilayani humo na kukagua shughuli za kiuchumi za wanawake wajasirimali.