Mkurugenzi wa shirika la afya Duniani kanda ya Afrika amezikosoa vikali nchi tajiri kwa kutoa chanjo ya tatu kwa watu ambao tayari wameshapatiwa chanjo hizo dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Mkurugenzi huyo Matshidiso Moeti amewaambia waandishi habari leo kwamba uamuzi wa nchi hizo unatishia mustakabali wa nchi za Afrika. Amesema kutokana na nchi tajiri kuhodhi chanjo swala la usawa wa chanjo linakuwa ni mzaha.
Amesema hali bado ni tete barani Afrika wakati ambapo maambukizi ya virusi vya aina ya Delta yanakuja juu katika nchi 54 za bara hilo. Mpaka sasa ni chini ya asilimia 2 ya watu bilioni 1.3 wa Afrika waliopatiwa chanjo.
Watu zaidi ya milioni 7.3 wameambukizwa virusi vya corona barani Afrika kote na 186,000 wamekufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.