Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linamshikilia Mohamed Jumaa (37) mkazi wa Kariakoo, kwa tuhuma za mauaji ya walinzi wawili waliofahamika kwa majina ya Eliakim Morali (30) mkazi wa Mbezi Beach na Saunkoo Bakari (35) mkazi wa Buguruni.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne imeeleza kuwa tukio hilo limetokea tarehe 26 mwezi huu majira ya jioni katika leneo la Tungi wilaya ya Kigamboni katika kituo cha mafuta cha JM.

Mohamed anadaiwa kuwagonga na kuwaua kwa makusudi walinzi hao na Lori lenye namba za usajili T 176 CVP.

Mtuhumiwa huyo ambaye ni mmiliki wa kituo hicho cha mafuta alikuwa na kesi ya madai namba 118/2018 Mahakama Kuu baada ya kushindwa kulipa mkopo kwa muda ndani ya muda unaotakiwa, ambapo licha ya kukata rufaa mara kadhaa mahakama ilitoa amri ya kuuzwa kwa kituo hicho cha mafuta.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea na
uchunguzi wa tukio hilo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu tuhuma zinazomkabili.