Ndugu zangu Waandishi wa Habari.
Leo nitakuwa na mambo kadhaa ya kuwapa taarifa kutoka Serikalini.

    Maendeleo ya bandari zetu katika Bahari na Maziwa Makuu.

Hali ya bandari zetu ni nzuri na zinaendelea kutoa huduma ya kusafirisha na kupokea mizigo ndani ya nchi na nje ya nchi, licha ya dunia kukabiliwa na janga ya ugonjwa wa Korona (Uviko-19). Biashara ya bandari inaendelea kukuwa kwa Watanzania na nchi jirani ambazo zinategemea bandari za Tanzania kutumia bandari zetu hasa Bandari ya Dar es Salaam.  


Katika miezi 6 iliyopita (Februari – Julai), bandari zetu zilizopo ukanda wa Bahari ya Hindi (Dar es Salaam, Tanga na Mtwara) na Bandari zilizopo katika maziwa yetu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) zimeongeza idadi ya meli zilizohudumiwa kutoka meli 1,388 (zilizohudumiwa katika kipindi hicho mwaka jana 2020) hadi kufikia meli 2,206. Halikadhalika kiwango cha shehena ya mizigo kimeongezeka kutoka tani Milioni 7.826 hadi kufikia tani Milioni 8.869.

Ongezeko kubwa tumelipata katika bandari yetu ya Dar es Salaam ambayo inafanya vizuri kwa kuongeza kiwango cha shehena ya mizigo kutoka tani Milioni 7.270 hadi kufikia tani Milioni 8.136.

Na tumefanya vizuri zaidi kwenye magari yanashushwa bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuingia nchini na mengi zaidi kwenda nchi jirani ambayo yameongezeka kutoka 64,209 ya mwaka jana (Februari – Julai) hadi kufikia 81,016 ya mwaka huu (Februari – Julai). Na hivi ndivyo biashara ya bandari inavyokua.

Kutokana na kuongezeka kwa biashara mapato ya bandari ya miezi 6 pia yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 525.4 hadi kufikia shilingi Bilioni 531.1. Mapato haya si haba, ziko baadhi ya nchi kutokana na changamoto ya Korona mapato ya bandari zao yameshuka kwa kiasi kikubwa lakini sisi hayakushuka.

Kwa upande wa maendeleo ya miundombinu ya bandari;

    Bandari ya Dar es Salaam


Kama mtakumbuka mwaka 2016 Serikali ilianza uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya takribani shilingi Trilioni 1. Uboreshaji huo umehusisha kuchimba kwa ajili kuongeza kina katika gati namba 1 – 7 (kuchimba kina cha hadi meta 14.5) na kujenga gati maalum iitwayo RORO ambayo ni kwa ajili ya kuhudumia meli za magari. Nafurahi kuwajulisha kuwa kazi hii imekamilika na gati zote zinatoa huduma.

Kutokana na uwekezaji huu wiki 3 zilizopita bandari yetu ya Dar es Salaam imeandika rekodi ya kupokea meli iliyoshusha idadi kubwa ya magari 3,743 ambayo haijawahi kutoka katika bandari za ukanda huu wa mashariki mwa Afrika.

Na kizuri zaidi hii imeonesha jinsi biashara ya Bandari ya Dar es Salaam inavyokuwa kwa kasi kwa sababu kati ya magari hayo asilimia 65 (2,945) ni yaliyokwenda nje ya nchi (nchi 6 zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam . Magari 798 ndio yalibaki nchini.

Kazi zinazoendelea sasa na zilizo katika mpango wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia na kugeuzia meli, kuboresha mtandao wa reli ndani ya bandari na kuongeza kina ili kuimarisha gati namba 8 – 11.

    Bandari ya Mtwara

Serikali imekamilisha ujenzi wa gati yenye urefu wa mita 300, imekarabati yadi ya kuhudumia mizigo yenye mita za mraba 5,600 na imekarabati ghala. Bandari ya Mtwara sasa inatumika na hivi karibuni imepokea meli kubwa iliyobeba viuatilifu aina ya sulphur tani 2,850 kwa ajili ya wakulima wa korosho.

    Bandari ya Tanga

Ujenzi wa gati mbili za Bandari ya Tanga unaendelea, na lengo la Serikali ni kuondoa usumbufu na gharama kubwa za kuhudumia meli zikiwa zimetia nanga mbali na gati. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika Oktoba mwakani (2022) kwa gharama ya shilingi Bilioni 256.8

    Bandari ya Nyasa

Serikali ipo katika hatua za mwisho za upembuzi yakinifu ili kuanza ujenzi wa gati za Mbambabay, Manda na Matema.

    Bandari ya Karema

Ujenzi wa bandari hii unaendelea, kwa sasa umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilila mwezi Machi 2022. Ujenzi huu utagharimu shilingi Bilioni 48 hadi kukamilika na matarajio ni kuwa bandari hii itasaidia kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na nchi za DRC na Burundi.

    Bandari ya Mwanza

Kama mnavyojua Serikali imekamilisha ujenzi wa chelezo yenye uwezo wa kubeba meli kubwa yenye uzito wa hadi tani 4,000 kwa gharama ya shilingi Bilioni 36.43. Chelezo hii inafanya kazi na hivi tunavyoongea meli ya MV Mwanza inaendelea kujengwa katika chelezo hii.

Kuhusu ujenzi wa Meli.

Ujenzi wa MV Mwanza (Hapa Kazi Tu) katika Ziwa Victoria unaendelea vizuri na umefikia asilimia 80. Meli itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo. Tayari Serikali imemlipa mkandarasi shilingi Bilioni 68.457 kati ya fedha zote za ujenzi wa meli hii ambazo ni shilingi Bilioni 89.764.

Mtakumbuka kuwa katika kuimarisha usafiri katika Ziwa Victoria Serikali imekamilisha ukarabati wa meli mbili za MV Victoria ambao umegharimu shilingi Bilioni 25.9 na MV Butiama uliogharimu shilingi Bilioni 5.88. Meli hizi zinafanya kazi vizuri kusafirisha abiria na mizigo na kukuza biashara katika ukanda wa ziwa.

Kwa sasa maandalizi ya ujenzi wa meli zinginye 4 na ukarabati wa meli 3 katika maziwa yetu makuu na bahari yanaendelea baada ya kusainiwa kwa mikataba Mwezi Juni, 2021. Miradi hii mipya itagharimu shilingi Bilioni 447.323.

  1.     Serikali itajenga meli mpya 1 ya abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika. Kwa shilingi Bilioni 104.7
  2.     Itajenga meli mpya ya mizigo yenye uwezo tani 2,700 katika Ziwa Tanganyika. Kwa takribani shilingi Bilioni 100.
  3.     Itajenga meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 2,800 katika bahari ya Hindi. Kwa shilingi Bilioni 129.8
  4.     Itajenga meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 3,000 za mabehewa katika Ziwa Victoria. Kwa shilingi Bilioni 84.6
  5.     Itakarabati meli ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika. Kwa shilingi Bilioni 8.5
  6.     Itakarabati meli ya mafuta ya MT. Nyangumi katika Ziwa Victoria na ukarabati wa meli ya uokozi na kuvuta matishari ya MT. Ukerewe. Gharama za miradi hii zinafanyiwa kazi na wakati wowote zabuni zitatangazwa.


    Maendeleo ya Shirika letu la Mawasiliano Tanzania (TTCL)

Kama mnavyojua Serikali imewekeza kiasi cha takribani shilingi Bilioni 600 katika Mkongo Mawasiliano wa Taifa kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa wananchi na pia kuzihudumia nchi jirani. (Biashara, nchi yetu inapata pesa)

Mkongo huu upo chini ya usimamizi wa Shirika letu la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na umeendelea kutoa huduma nzuri iliyoleta nafuu kubwa ya mawasiliano nchini mwetu.

Sasa kazi ya upanuzi wa huduma ya mkongo wa Taifa inaendelea vizuri, kazi inayoendelea sasa ni ya kuunganisha mkongo kutoka Singida kwenda Mbeya kutia Kambikatoto.

Pia kuna ujenzi wa Mkongo wa Taifa kutoka Mtambaswala kwenda Msumbiji (tunakwenda kufanya biashara na Msumbiji).

Msumbiji itakuwa nchi ya 7 kuhudumiwa na Mkongo wa Taif awa Tanzani, tayari huduma za mkongo wa Taifa tumeshazipeleka Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda, Kenya na DRC. Na pia tunaangalia kupeleka Uganda.

Nafurahi pia kuwajulisha kuwa Serikali kupitia TTCL imefanikiwa kuongeza uwezo wa huduma za mawasiliano inayoipatia nchi ya Rwanda kutoka 1.24GBPS hadi 2.5 GBPS. Maana yake ni kwamba Rwanda italipa zaidi kwa Tanzania. Tunapata fedha za maendeleo.

Nyote mnafahamu kumekuwa na malalamiko ya Watanzania katika baadhi ya maeneo ya vijijini kulalamikia kukosa huduma za Mawasiliano kutokana na kampuni za mawasiliano za simu kukataa kupeleka huduma huko. Kwa kutambu hilo TTCL imejenga minara mipya 60 na itaongeza minara mipya 100 ili kuwafikia wananchi hao. Kila mtanzania ana haki ya kuwasiliana na mawasiliano ni maisha

Ndugu zangu waandishi wa habari ningependa kufafanua kidogo kuhusu faida za Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. Ni kutokana na kuwepo kwake nchi yetu imekuwa moja ya nchi 5 Barani Afrika zenye gharama za chini za bando za Internet. Tanzania hivi sasa inazizidi hadi baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuwa na huduma za Internet zenye gharama nafuu.

Mfano leo Mtanzania ana uwezo wa kupata GB1 kwa chini ya shilingi 2,000 lakini zipo nchi ambazo GB moja inauzwa hadi Dola 20 za Marekani yaani hapo unazungumza zaidi ya shilingi 45,000.  Kwa hiyo Mkongo huu umetuletea manufaa makubwa sana sisi wananchi achilia mbali fedha ambazo nchi inapata kwa kupeleka huduma hiyo katika nchi jirani.

    Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona (Uviko-19)

Serikali inaendelea kuwahimiza wananchi kuzingatia tahadhari zote za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa korona (Uviko-19), kupata chanjo ambazo zinaendelea kutolewa katika vituo mbalimbali nchi nzima. Mpaka sasa watu zaidi ya 300,000 wameshapata chanjo na zoezi linaendelea vizuri.

Kulikuwa na changamoto kidogo mipakani, lakini sasa hivi changamoto zimetatuliwa. Katika mipaka yetu yote wananchi wanapimwa kile kipimo cha haraka bila kulipia. Na hii inafanyika ili kurahisisha biashara na shughuli nyingine za wananchi baina ya nchi zetu.

Pia kulikuwa na malalamiko ya gharama za vipimo kwa wasafiri waendao nje ya nchi hasa kwenye viwanja vyetu vya ndege, lakini sasa tatizo limetatuliwa kwa kupunguza gharama za kipimo cha haraka kutoka Dola za Marekani 25 hadi 10, na kile kipimo kiitwacho PCR ambacho baadhi ya hudai kitumike kimepunguzwa kutoka Dola za Marekani 100 hadi 50.

Serikali inaendelea kuwahimiza Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19, kwa sababu ugonjwa huu upo na unawaathiri watu na kusababisha vifo.

Na hapa nina ujumbe wa Mhe. Innocent Bashungwa (Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) anawasihi ndugu zangu waandishi wa habari kujitokeza kupata chanjo kwa sababu majukumu yetu yanatuweka katika hatari ya kuambukizwa Uviko-19.

    Agizo la Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kurudishwa kazini.

Wiki hii kulitokea hali ya sintofahamu kidogo baada ya mtumiaji wa mitandao mmoja kueneza habari kuwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa katangaza kuwa watumishi walioondolewa kazi kutokana na kukutwa na vyeti feki wamerudishwa kazi.

Taarifa hii ni ya upotoshaji. Alichokisema Mhe. Waziri Mkuu ni kuwa Watumishi 4,380 waliorudishwa kazini ni wale walioondolewa kimakosa mwaka 2017. Na hawa ni wale watumishi ambao waliajiriwa kabla ya mwaka 2004 wakiwa na sifa ya darasa la saba. Pia Mhe. Waziri Mkuu akaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasilisha orodha ya Watumishi ambao wana sifa ya kurudishwa ili wafanyiwe kazi.

Kwa hiyo sio kweli kwamba Mhe. Waziri Mkuu kaagiza watumishi walioondolewa kwa vyeti feki warudishwe kazini kama inavyoenezwa.

    Maendeleo ya miradi ya kimkakati

    Usafiri wa anga.


Ndege zetu zinaendelea kutoa huduma za ndani ya nje ya nchi. Zikiimarisha biashara, uwekezaji na utalii.

Mtakumbuka niliwaeleza juu ya mpango wa kununua ndege nyingine 5. Nafurahi kuwaeleza kuwa malipo ya awali ya kununua ndege hizo yameshafanyika, tayari Wataalamu wetu wameshachagua muonekano wa ndege zetu na ndege hizi zinatarajiwa kuwasili hapa nchini kwetu mapema mwaka 2023.

Kwa upande wa huduma ni kwamba pamoja na kutoa huduma katika vituo 23 vya ndani na nje ya nchi, tayari Shirika letu la ndege la ATCL limerejesha safari zake za kwenda India (zinaanza kesho), linasafirisha mizigo kwenda China na hivi karibu litaanza kwenda Nairobi, Kenya na Lubumbashi, DRC.

    Ujenzi wa Reli (SGR).

Ujenzi unaendelea vizuri. Dar es Salaam – Morogoro tumefikia asilimia 93, na Morogoro Makutupora tumefikia asilimia 67.65

Mwishoni mwa Novemba mwaka huu tunatarajia kupokea Injini 2 na Mabehewa 12 ya Treni ya majaribio katika njia yetu mpya ya SGR. Mabehewa mengine 18 yanatarajiwa kuwasili nchini ifikapo Juni 2022. Pia kuna mabehewa mengine 59 yatafika mwaka 2023.

Pia kuna treni za vichwa vya umeme 10 na mabehewa yake 80. Hizi ni zile treni zenye vichwa huku na huku (zinaitwa EMU-Electrical Multiple Unit).

Lakini kwa sasa muda wowote Dar es Salaam na Morogoro itaungana na treni ya wakandarasi ambayo kwa sasa inatembea kati ya Ngerengere na Pugu itaweza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

    Ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere katika mto Rufiji

Ujenzi unaendelea vizuri, kwa sasa kazi zimefikia asilimia 57. Kwa kuwa mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni mwakani, Serikali kupitia TANESCO inaendelea na manunuzi ya vifaa mbalimbali vikiwemo Transifoma, Mashine za kufulia umeme na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka ulipo mradi hadi Chalinze ambako itaungana na Gridi ya Taifa. Malipo ya wakandarasi yanakwenda vizuri.

    Ujenzi wa Viwanja vya ndege.

Ujenzi wa viwanja 11 vya ndege unaendelea vizuri, na kazi zimefika katika viwango mbalimbali;

    Uwanja wa ndege wa Mtwara umefikia asilimia 70 – Bilioni 55.2

    Uwanja wa ndege wa Songea umefikia asilimia 94 (njia ya kutua na kuruka ndege imekamilika na inatumika) – Bilioni 37.

    Uwanja wa Kimataifa wa Songwe umefikia asilimia 55 – Bilioni14.7.
    Uwanja wa ndege wa Iringa (Nduli) umefikia asilimia 25 – Bilioni 41.

Na viwanja vingine vikiwemo Musoma, Sumbawanga, Shinyanga, Tabora na Kigoma kazi zinatarajiwa kuanza wakati wowote.

    Ujenzi wa miundombinu ya Dar es Salaam

Kama mnavyojua Dar es Salaam ni Jiji la Kibiashara. Serikali ilitupa jicho la kimkakati la kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya barabara, madaraja ya juu na chini. Ujenzi unaendelea vizuri katika maeneo mbalimbali.

Mifano michache ni:

    Upanuzi wa barabara ya Morogoro kwa lengo kurahisisha uingiaji na utokaji wa ndani ya Jiji ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam. Ujenzi wa kilometa 19 za barabara ya njia nane kuanza Kimara hadi Kibaha kazi imefikia asilimia 93.

    Flyover ya Chang’ombe ujenzi umefikia asilimia 44, Flyover ya Kurasini ujenzi umefikia asilimia 45, Overpass (njia ya kukatiza juu) kule bandarini imefikia asilimia 13.

    Mradi wa ujenzi wa Awamu ya Pili ya barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) kipande cha kwanza 1 (Hii ni barabara ya Kilwa inaanzia Mbagala – Kariakoo kisha inaanzia Changombe JKT kupitia barabara ya Kawawa hadi Magomeni. Lakini pia inaanzia Gerezani kuzunguka Water Front, Centra Polisi hadi Posta) imefikia asilimia 25. Kipande cha 2 cha mradi huu kinachohusisha ujenzi wa majengo Mbagala na Vituo vya kupakia na kushusha abiria kutoka nje ya barabara, kazi hii imefikia asilimia 95.

    Ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo – Busisi)

Ujenzi unaendelea vizuri, hadi sasa umefikia asilimia 28. Matarajio ya ujenzi wa daraja hili lenye urefu wa kilometa 3.2 na litakalogharimu takribani shilingi Bilioni 700 unatarajiwa kukamilika Julai 2023.

    Katika Sekta ya Elimu.

Ningependa kuzungumza elimu ya juu.

Kama mnavyojua katika mwaka huu wa fedha Serikali iliamua kuongeza bajeti katika mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi Bilioni 464 mwaka uliopita hadi kufikia shilingi Bilioni 570. Ongezeko hili limewezesha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa kunufaika na mikopo kutoka 149,398 hadi kufikia wanafunzi 160,000.

Nafurahi kuwajulisha kuwa tangu kufunguliwa kwa dirisha la mikopo mwaka huu hadi tarehe 27 Agosti, 2021 wanafunzi 88,694 wameomba mikopo na wengine wanaendelea kuomba hadi mwisho wa dirisha la mikopo hiyo tarehe 31 Agosti, 2021.

    Ukusanyaji wa mapato.

Hali ya ukusanyaji wa mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuimarika. Kwa takwimu za Mwezi Julai 2021 TRA imefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.535 sawa na asilimia 97.4 ya lengo. Kiasi hiki ni kikubwa ikilinganishwa na makusanyo ya mwezi Julai mwaka jana ambapo ilikusanya shilingi Trilioni 1.284 sawa na asilimia 84.1 ya lengo. Ukusanyaji huu hauhusiani na tozo za miamala ya simu.

Serikali inawapongeza Watanzania wote kwa kuitikia kulipa kodi bila shuruti, na inaendelea kuimarisha mazingira ya uzalishaji na ufanyaji biashara ili kodi iongezekezeke kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mwezi huu wa Julai 2021 TRA pia imeanza kukusanya kodi ya majengo kupitia Luku (mita za umeme), ambapo kila nyumba ya kawaida inalipiwa shilingi 1,000 kwa mwezi na kila sakafu ya nyumba ya ghorofa inalipiwa shilingi 5,000 kwa mwezi. Zoezi hili limeanza na matarajio ni kukusanya shilingi Bilioni 46.517 kwa mwaka huu 2021/22.

Kwa kuwa ni zoezi jipya, TRA kwa kushirikiana na TANESCO wanafanyia kazi baadhi ya changamoto ikiwemo kuwataka wamiliki wa nyumba kujitokeza.

Naomba kusisitiza kuwa lengo la kuanzisha utaratibu huu ni kupunguza changamoto kubwa iliyowakumba wananchi walioshindwa kulipia kodi ya nyumba na kujikuta wanaangukia katika faini kubwa (unakuta mtu aliyetakiwa kulipia shilingi 10,000 anakumbana na faini na kulipishwa shilingi 70,000). Lakini pia inarahisisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza gharama kubwa za kukusanya mapato hayo.

     Mwongozo wa uendeshaji wa akaunti za mitandao ya kijamii ya Serikali.

Kama mnavyojua mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano. Kwa kutambua hilo, Idara ya Huduma za Habari (MAELEZO) tumeandaa mwongozo wa jinsi akaunti za mitandao ya kijamii za Serikali zitakavyoendeshwa.

Naomba kuutambulisha mwongozo huo leo na niwaombe Maafisa na Viongozi wa Serikali wanaoendesha mitandao ya kijamii ya Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuzingatia mwongozo huu.

Lengo letu ni kuhakikisha utoaji taarifa za Serikali kupitia mitandao ya kijamii unazingatia Sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali ya utoaji taarifa badala ya kila Afisa kufanya anavyotaka yeye. Tunataka kuepusha kuweka maudhui yasiyofaa katika akaunti rasmi za Serikali.

Pamoja na mwongozo huu, Serikali inaendelea kuhakikisha akaunti rasmi zote zinathibitishwa (Verification) ili ziweze kuaminiwa.

Natoa wito kwa Maafisa Habari wote wa Serikali na viongozi kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa sababu hii ni njia muhimu ya kuwasiliana na wananchi.

    Michezo

Kwenye michezo kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya kuziandaa timu za Taifa, na wote mnafahamu Mhe. Samia Suluhu Hassan Mwanzoni mwa wiki amekutana na timu ya soka ya vijana chini ya miaka 23 na wanariadha waliotuwakilisha kule Tokya Japan, na amewahakikishia juu ya dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika michezo.

Kwa sasa Serikali inafanya maandalizi ya Michuano ya Taifa (Taifa Cup) inayotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu 2021.

Baada ya kusitishwa kwa muda mrefu, Michuano ya Shule za Msingi (UMITASHUMITA) na Michuano ya Shule za Sekondari (UMISETA) imerudishwa na mpango wa Serikali ni kuiboresha zaidi mwakani ili kuendelea kuibua vipaji vya vijana wetu.