Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Kampuni ya Uwekezaji ya Pamoja-UTT-AMIS kutoa elimu zaidi ya uwekezaji kwa wananchi wakiwemo wastaafu wanaokabiliwa na changamoto kubwa ya kufanya uwekezaji wa mafao yao ya uzeeni kwenye miradi isiyo na tija na kuwasababishia hasara.

Mheshimiwa Masauni alitoa maagizo hayo alipotembelea Taasisi ya UTT-AMIS inayosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Taasisi zinazosimamiwa na Wizara hiyo, Jijini Dar es Salaam

Alisema kuwa uwekezaji kwenye mifuko inayosimamiwa na UTT-AMIS umekuwa na tija kubwa na kwamba licha ya mfuko huo kufanya vizuri na kutoa faida inayomnufaisha mwekezaji, watu wengi hawana taarifa muhimu kuhusu mfuko huo na kuuagiza uongozi kuongeza kasi ya kujitangaza.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko huo unaoendesha mifuko 6 ya uwekezaji, ukiwemo mfuko wa Umoja, Wekeza, Watoto, Jikimu, Ukwasi na Hati Fungani, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT-AMIS, Bw. Simon Migangala, alisema kuwa mfuko wake umefanikiwa kuongeza mtaji kutoka shilingi bilioni 290.7 hadi shilingi bilioni 619.6 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mwisho