Mashirika ya kimataifa ya kiutu yameonya kuwa mamilioni ya watu wa Syria na Iraq wapo katika kitisho cha kukosa upatikanaji wa maji, umeme na chakula katikakati mwa ongezeko la joto, kiwango kidogo cha maji na ukame. 

Nchi hizo mbili jirani ambazo kwa miaka mingi zimekabiliwa na migogoro na usimamizi mbovu, zinahitaji hatua za haraka katika kushughulikia uhaba mkubwa wa maji. 

Ukame pia umevuruga usambazaji wa umeme wakati kiwango cha chini cha maji kikiyaathiri mabwawa na miundombinu muhimu ikiwemo vituo vya afya. 

Zaidi ya watu milioni 12 katika nchi zote mbili wameathirika wakiwemo watu milioni 5 nchini Syria ambao wanategemea moja kwa moja maji kutoka mto Euphrates. 

Carsten Hansen mkurugenzi wa kikanda wa shirika la wakimbizi la Norway amesema maelfu ya Wairaqi bado hawana makaazi na wengine wengi wanakimbia kutoka Syria.