Rais wa zamani wa Afrika Kusini anayetumikia kifungo cha miezi 15 jela Jacob Zuma amefanyiwa upasuaji Hospitalini lakini hadi sasa haijawekwa wazi ni upasuaji wa nini ila ataendelea kusalia Hospitalini kwa ajili ya operesheni nyingine alizopangiwa.

Taarifa ya Msemaji wa Idara ya Magereza Singabakho Nxumalo imeeleza kwamba Zuma alifanyiwa upasuaji jana Jumamosi na taratibu nyingine zimepangwa kwa ajili yake katika siku zijazo.

Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu uwezekano wa kuachiwa kwa Zuma ambaye anapinga kifungo chake gerezani.

Zuma anayetumikia kifungo cha miezi 15 gerezani katika gereza la Estcourt kwa kosa la kuidharau Mahakama, alipelekwa hospitali Agosti 6 kwa ajili ya uchunguzi, siku chache kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya rushwa inayomkabili.