China imeijibu Marekani ikiituhumu kwa kujificha nyuma ya maneno matupu ya utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria ili kuitetea tabia yake ya uonevu na ya ujinga. 

Hii ni baada ya Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris kuituhumu China kwa kutoa vitisho barani Asia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China Wang Wenbin amesema hatua ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan ni mfano wa sera ya kichoyo ya kigeni ya Marekani. 

Akizungumza mapema leo nchini Singapore, Harris ameituhumu China kwa kutumia nguvu na vitisho ili kuhalalisha madai yake yasiyo halali ya kumiliki Bahari ya Kusini mwa China. 

Ziara yake ya siku saba nchini Singapore na Vietnam, ambayo ni ya pili kimataifa, inalenga katika kudhibiti ushawishi unaoongezeka wa China wa kiusalama na kiuchumi na kuonyesha kuwa Marekani inaweza kuongoza njia.