Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameamuru wabunge Josephat Gwajima na Jerry Silaa kupelekwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Taarifa iliyotolewa na bunge imeeleza kuwa tuhuma zinazowakabili wabunge hao ni pamoja na kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya bunge.

Gwajima ambaye ni mbunge wa Kawe anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo inayochunguza mambo yanayohusu maadili ya wabunge yanayopelekwa na spika, Agosti 23 huku Silaa ambaye ni Mbunge wa Ukonga akitakiwa kufika mbele ya kamati Agosti 24.

Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa endapo watajwa au mmoja wao hatoitikia wito huo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Hata hivyo, bunge halijaeleza ni makosa gani wabunge hao wanadaiwa kutenda na kupelekea kushusha hadhi na heshima bunge.