Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga), wamepewa adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili mfululizo  ya Bunge, baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya kudharau na kudhalilisha mhimili huo.

Adhabu hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 31 Agosti 2021, bungeni jijini Dodoma,  baada ya wabunge kuunga mkono adhabu zilizopendekezwa na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge, dhidi ya wabunge hao.

Wabunge hao wiki iliyopita waliitwa mbele ya kamati hiyo kwa kuhojiwa kuhusu matamshi waliyotoa nje ya Bunge.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka ameliambia Bunge kuwa wawili hao ni wakaidi na wajeuri lakini ni watu ambao hawakutaka kujutia kauli zao.

Mwakasaka amesema wabunge hao mbali na adhabu walizopewa, lakini wanatakiwa kuangaliwa kuhusu mienendo yao nje ya Bunge.

Kwa upande wa Askofu Gwajima amepewa adhabu hiyo huku alitakiwa kuchunguzwa na vyombo vingine kutokana na kinachodaiwa ni uchochezi na upotoshaji.

Kamati imependekeza Gwajima pia kufikishwa mbele ya kamati ya chama chake CCM ili akahojiwe huko kuhusu mwenendo wake.

Kwa upande wake Silaa kamati imependekeza asimamishwe mikutano miwili lakini avuliwe uwakilishi wa Bunge la Afrika (PAP) kwa madai anaweza kusema uongo huko.

Kilichomponza Silaa ni kauli yake kuwa wabunge hawalipi kodi katika mishahara yao jambo lililoelezwa ni uongo kwani wabunge wanalipa kodi.