Embe ni tunda linalofahamika na kupendwa na watu wengi. Watu hula tunda hili moja kwa moja au kulitumia kutengeneza sharubati (juice).

Kwa hakika ikiwa haupendi au haufahamu umuhimu wa tunda hili katika afya yako ni wakati wa kujifunza kitu sasa.

1. Huboresha metaboli
Embe ni tunda lenye nyuzinyuzi kwa kiasi kikubwa. Nyuzinuzi zinahitajika sana katika kufanya mchakato wa metaboli (mwili kutumia vrutubisho kujipa nguvu) kwenda vizuri.

2. Huboresha afya ya macho
Kula embe kutakunufaisha kwa kulinda macho yako dhidi ya kudhoofu kwa misuli ya macho. Embe ni chanzo kizuri cha vitamini A ambayo ni muhimu kwa ajili ya macho.

3. Huweza kuzuia saratani
Tunda la embe limesheheni kemikali kama vile methylgallat, astragalin, isoquercitrin, fisetin, quercetin na gallic acid ambazo kwa pamoja zinazuia kutokea kwa maradhi ya saratani. Utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa pectin inayopatikana kwenye maembe huvuruga utendaji kazi wa galectin 9 ambayo hupatikana kwenye seli za saratani

4. Husaidia kukabili kisukari
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ulaji wa embe huweka kiwango cha mwili cha sukari na insulini katika hali nzuri.

5. Hukabili shinikizo la damu mwilini
Madini ya potasiamu yanayopatikana kwenye embe huasidia dosari zinazosababishwa na madini ya sodiamu katika damu. Potasiuam hurekebisha nguvu ya msukumo wa damu (blood pressure) na kuufanya uwe wa kawaida.

6. Huongeza alkaline mwilini
Asidi za tartaric na malic inazopatikana kwenye embe huongeza kiwango cha alkaline mwilini. Alkaline ni muhimu kwani husaidia kuzuia maradhi ya figo pamoja na udhaifu wa mifupa. Alkaline husaidia pia kuwezesha usafirishaji wa oksijeni katika mwili mzima.

7. Hutumika kama kipodozi cha nywele
Kwa kuchanganya ujiuji wa embe, yai pamoja na kijiko kimoja cha asali, na yogurt; unaweza kupata kipodozi kizuri kwa ajili ya nywele zako. Paka mchanganyiko huu na subiri kwa muda wa dakika thelathini kabla ya kuosha nywele zako.

8. Hupunguza lehemu (cholesterol) mwilini
Kiwango cha mafuta ya lehemu kikizidi ni hatari kwa ajili ya afya ya moyo. Vitamini C pamoja na pectin inayopatikana kwenye embe huuwezesha mwili kujikinga na athari za lehemu.

9. Hukabili maradhi ya shambulio la moyo
Madini ya potasiamu yanayopatikana kwenye embe ni muhimu kwa ajili ya afya ya misuli ya moyo. Hivyo kunywa sharubati (juice) ya embe au kula matunda ya embe mara kwa mara kutakukinga na hatari ya maradhi ya shambulio la moyo.

10. Ni chanzo kizuri cha madini ya chuma
Embe ni chanzo kizuri cha madini ya chuma ambayo ni muhimu kwako ili kujikinga na maradhi kama vile anemia.

11. Huboresha kinga mwili
Kinga mwili inahitaji vitamini A na C ili kujijenga na kujiimarisha. Hivyo ulaji wa matunda ya embe utakupatia vitamini hizi zinazopatikana kwenye matunda haya kwa wingi.

12. Ni chanzo cha asidi ya folic
Asidi ya folic inayopatikana kwenye embe katika mfumo wa vitamini B ni muhimu sana kwa afya ya mama mjamzito na mtoto. Inashauriwa na wataalamu wa afya kula tunda la embe hasa kwa wajawazito.

13. Huboresha mmeng’enyo wa chakula
Embe lina enzyme ambazo husaidia katika uvunjwaji na uchakatwaji wa protini mwilini. Pia kama nilivyosema pale awali kuwa embe lina nyuzinyuzi ambazo ni muhimu katika kumeng’enya chakula.

14. Husaidia katika afya ya ngozi
Embe ni muhimu kwa ajli ya afya ya ngozi kwani lina beta-carotene ambayo mwili huibadili kuwa vitamini A na lina vitamini C kwa wingi ambazo zote kwa pamoja ni muhimu kwa ajili ya afya ya ngozi.

15. Huboresha uwezo wa kumbukumbu
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika jarida la Oxidative Medicine and Cellular Longevity, unaeleza kuwa embe lina vitamini B6 pamoja na asidi ya glutamine ambavyo vyote kwa pamoja huboresha afya ya ubongo.