Vikosi vya kuzima moto nchini Algeria vimeendelea na juhudi za kudhibiti moto unaowaka kwenye maeneo 19 kaskazini mwa nchi hiyo, ambako watu 90 walipoteza maisha wiki hii kutokana na janga hilo.
Taarifa kutoka idara ya huduma za dharura imesema wazima moto wanajaribu kwa nguvu zote kuuzima moto huo unaowaka kwenye majimbo 9.Idara hiyo imesema moto unawaka kwenye maeneo 6 huko Bejaia, maeneo matatu katika jimbo la El Tarf na umeripotiwa pia kwenye maeneo mawili ya jimbo la Tizi Ouzou.
Eneo la Tizi Ouzou ndiyo limeathiriwa vibaya zaidi na moto na ripoti zinasema vijiji vingi vimeteketea. Serikali imesema moto huo umewashwa na watu na kiwango cha juu cha joto kaskazini wa Ageria kimefanya iwe vigumu kuudhibiti. Kumbukumbu zinaonesha mwaka uliopita lilitokea janga kama hilo ambapo hekta 44,000 ziliteketea.