KLABU ya Yanga imetozwa faini ya Sh. milioni 3, 850,000 kufuatia makosa mbalimbali waliyoyafanya katika mchezo wao wa ugenini wa kiporo namba 208 wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliochezwa Julai 3 dhidi ya Watani wao wa Jadi, Simba.

Katika mchezo huo Yanga walifanikiwa kupata goli lililofungwa dakika ya 12 na Zawadi Mauya lililodumu hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika na kuwazuai Simba kutangaza ubingwa kutumia mgongo wao.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyoketi Julai 6 kupitia mwenendo wa matukio mbalimbali ya Ligi Kuu na Kufanya maamuzi imeweka wazi kuwa, katika mshezo huo Yanga walitumia mageti ya uwanja wa Uhuru kuingia uwanja wa Benjamin Mkapa badala ya mlango maalumu unaotumiwa na timu.

Katika kosa la pili, timu hiyo ilitumia mlango wa chumba cha waandishi wa habari badala ya mlango maalumu unaotumiwa na timu huku pia wakiingia uwanjani kupasha misuli joto ‘Warm up’, kwa kutumia mlango ambao haukupangwa kutumika kwa namna yeyote.

Pia Yanga ilitenda kosa lingine kwa kutumia chumba cha wafanya usafi wa uwanja huo kwa ajili ya kubadilishia nguo baadala ya chumba maalumu walichotakiwa kutumia.

Mbali na makosa hayo manne lakini pia Yanga imetakiwa kulipa faini ya Sh. 850,000 ikiwa ni gharama ya ukarabati wa mageti yaliyovunjwa wakati wakiiingia uwanjani pamoja na makufuli ya uwanja wa Benjamin Mkapa yaliyoharibiwa katika tukio hilo adhabu ambazo zimetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 15(15) ya Ligi Kuu kuhusu tartibu za mchezo.