Klabu ya Yanga imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Watani wao wa Jadi, Simba SC katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa ukishududiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan .

Bao pekee la Yanga SC lilifungwa na Kiungo wa Klabu hiyo, Zawadi Mauya dakika ya 11 ya mchezo baada ya kupiga shuti kali lililomgonga Beki wa Simba SC, Shomari Kapombe na kutinga wavuni likiwaacha Simba wakishangaa dakika za mwazo za mchezo huo.

Yanga SC walionekana kuzuia kwa kuwa wengi golini kwao dakika zote huku wakitumia mchezo wa kushambulia kwa kushtukiza .

Mabeki wa pembeni wa Yanga SC, Kibwana Shomari na Adeyum Salehe walionekana kumbana vilivyo Mchezaji  wa Simba SC, Bernard Morrison na kukosa nafasi ya kufurukuta katika mchezo huo licha ya ubora wa safu ya Kiungo kikiongozwa na Clatous Chama.

Simba SC imeshindwa kutangaza Ubingwa wa Ligi Kuu Bara (VPL) mbele ya Yanga SC sasa itasubiri michezo yake iliyobaki katika Ligi hiyo dhidi ya Azam FC, Namungo FC, Coastal Union na KMC FC.