WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Tanzania na Burundi wafanye kazi kwa kuzingatia weledi na uaminifu mkubwa huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa.

“Mataifa yetu yako kwenye ujenzi wa uchumi ni lazima kwa kila mmoja wetu afanye kazi kwa bidii. Waliopo maofisini, mashambani na viwandani wote kwa pamoja tuchapeni kazi.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Alhamisi, Julai Mosi, 2021) alipotembelea kiwanda cha kutengeneza mbolea cha FOMI kilichoko jijini Bujumbura nchini Burundi.

Waziri Mkuu jana alimuwakilisha Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa Burundi, baada ya hafla hiyo alitembelea kiwanda hicho.

“Kilichinivutia kuja hapa ni mabadiliko yanayofanywa na Rais wenu Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye na leo nchi inaonekana kwenda mbio kwenye maendeleo hasa ukuaji wa uchumi.”

“…Wana-Burundi si rahisi nyinyi kuyaona mabadiliko mnayoyafikia sisi tuliopo nje ya nchi ya Burundi ndiyo tunawaona mnavyobadilika kimaendeleo, endeleeni kuchapa kazi,” awalisisitiza.

Waziri Mkuu alisema mahitaji ya mbolea Tanzania ni zaidi ya tani 700,000 na nchi inatumia fedha nyingi kuagiza kutoka nje hivyo amemkaribisha mwekezaji huyo kuja kuwekeza nchini.

Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Wana-Burundi waje wawekeze na kufanya biashara nchini kwa sababu kuna ardhi kubwa na nzuri, umeme wa uhakika na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Waziri Mkuu ambaye aliambatana na Waziri wa Kilimo wa Burundi Deo Guide Rurema kiwandani hapo alisema Tanzania na Burundi si majirani ni ndugu wa baba na mama mmoja.

Alisema undugu huo uliasisiwa na viongozi wa kwanza wa mataifa hayo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwanamfalme, Louis Rwagasore. “Jukumu letu ni kuienzi tunu hii.”

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU