Waziri Mkenda Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Mkurugenzi Mkaazi Wa Usaid Tanzania
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Mb) Tarehe 9 Julai 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Ndg Andy Karas katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo Mhe Mkenda amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ili kuondokana na dhana ya kilimo cha kujikimu na kuhamia katika kilimo cha kibiashara. Waziri Mkenda amesema kuwa ili kuongeza tija katika Kilimo, Serikali imejipanga kuimarisha utafiti.
Amesema kuwa maendeleo ya kilimo yanategemea zaidi utafiti hususani wa udongo vilevile kubaini teknolojia bora itakayo pelekea kukisogeza kilimo katika hatua kubwa ya mafanikio na kimageuzi.
Amesema kuwa pamoja na mambo mengine wizara ya kilimo pia imejipanga katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kuliko kusafirisha pasina kuongeza thamani.
“Tukiongeza thamani ni wazi kuwa uchumi utapanda, lakini zaidi ajira ziataongezeka kwa wananchi, tutakuwa na Pato zuri la kigeni sambamba na utambulisho wa nchi” Alikaririwa Mhe Mkenda
Kuhusu sekta ya umwagiliaji Mhe Mkenda amesema kuwa Tanzania ina jumla ya Hekta zaidi ya Milioni 29 zinazofaa katika umwagiliaji lakini ni hekta zisizofikia hata milioni moja ndizo ambazo zimefanyiwa kazi.
“Kwa maana hiyo kuna fursa kubwa katika umwagiliaji hivyo ninyi kama wadau kadhalika natoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwekeza katika umwagiliaji” Amesema
Kuhusu Lishe Waziri Mkenda amesema kuwa wizara imeendelea kuweka hamasa kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusisitiza umuhimu wa kusisimamia kwa weledi tija katika mazao hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Ndg Andy Karas ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini.