Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wakandarasi wanaojenga miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupeleka umeme katika maeoneo maalum ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo wakati akizindua Mradi wa Ujazilizi Umeme Vijijini Fungu la Pili A ngazi ya mkoa uliofanyika Julai 29,2021 katika kijiji cha Mheza wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro.

Aidha, amewakumbusha  viongozi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya kata na vijiji kutenga maeneo maalum ya uwekezaji wa viwanda ili yaweze kupelekewa miundombinu ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini. “Tumieni umeme kufanya biashara muongeze thamani ya mazao ya kilimo na mifugo kwa kuanzisha viwanda” alisisitiza.

Waziri Kalemani amesema Mradi huo utatekelezwa kwa muda miezi 12 na Serikali imetenga  kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 8.59 kwa ajili ya kuvifikishia umeme vitongoji ambavyo havina umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro katika fedha hizo Wilaya ya Same imetengewa zaidi ya Shilingi Bilioni 3.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango Malecela ameishukuru Serikali kwa kupelekewa miradi hiyo ya kusambaza umeme vijijini na kuomba maeneo ambayo bado hayajafikishiwa umeme yapatiwe nishati hiyo.