Na. Steven Nyamiti, Kagera
Waziri wa Madini Doto Biteko amemuagiza Meneja Mkuu wa Mgodi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bodi na Menejimenti pamoja na wafanyakazi wote wa mgodi wa STAMIGOLD, kujitafakari kama utendaji wao una manufaa kwa Taifa.

Amesema hayo Julai 13, 2021 Biharamulo Mkoani Kagera katika ziara aliyoifanya ya kutembelea mgodi wa STAMIGOLD ambayo ni Kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) uliyopo katika wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera.


Akizungumza na menejimenti pamoja na wafanyakazi wa mgodi wa STAMIGOLD amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inachukizwa sana na vitendo vya utoroshaji madini ya dhahabu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wasiowaaminifu.

“Mungu amewapa bahati ya kuwa kwenye mgodi huu nawasihi uleeni mgodi huu. Mkiulea na nyinyi utawalea. Shirika hili likifa wengi mtapoteza ajira na kukosa mishahara” ameeleza Waziri Biteko.

Waziri Biteko amemuagiza mwenyekiti wa bodi ya STAMICO kuhakikisha anachukua hatua za kiutumishi dhidi yao na wale waliopo mahakamani hatua za ndani zifuatwe za kazi ili wawajibishwe.

Naye, Meneja Mkuu wa mgodi wa STAMIGOLD Injinia Gilay Shamika akieleza taarifa ya Maendeleo ya mgodi huo hadi kufikia Mwezi Mei 2021 amesema wafanyakazi wote wa mgodini kwa sasa wanafanya kazi kwa kujituma kwa kila hali ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha hawarudi nyuma tena katika kuilinda rasilimali madini katika mgodi huo.

Aidha, Injinia Shamika ameipongeza STAMICO kwa kuendekea kufanikisha shughuli mbalimbali za Uwekezaji za mgodi wa STAMIGOLD.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko alitembela na kujionea miundombinu iliyopo katika mgodi wa STAMIGOLD ikiwemo mtambo wa uchenjuaji wa Dhahabu na Bwawa la kuhifadhia topesumu (TSF).Pia Waziri Biteko ametembelea Mgodi wa wachimbaji wadogo wa Dhahabu Matwiga ambapo amezungumza na wachimbaji wa eneo hilo kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzitolea majibu.

Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Mkuu wa wilaya ya Biharamulo Kimelembe Rwota, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita Lucas Mlekwa, Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Madini Ramadhani Lwamo, Kaimu kamishna wa madini Muhandisi Zephania Nsungi na wafanyakazi wa STAMIGOLD.