Na WAMJW - Moshi, Kilimanjaro.
Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wametakiwa kuhakikisha wanatumia kadi za uanachama wao katika kufanya malipo halali ya huduma wanazopata katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alipokuwa ziara katika Mkoa wa Kilimanjaro na kupokea ripoti ya ubadhirifu wa NHIF unaofanywa na wanachama pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya.

"Kila Mtanzania ahakikishe kadi yake ya bima ya afya inatumika kufanya malipo halali tuu, kila mwenye duka la dawa ahakikishe anaposaini fomu za bima ya afya na anapopokea na kudai madai, adai malipo halali tuu" amesema Dkt. Mollel

Dkt. Mollel amezitaka taasisi za umma na binafsi zinazotoa huduma za afya nchini kuhakikisha kadi za bima ya afya zinatumika kwenye malipo halali huku wakiwasimamia vyema watumishi hao wasijiingize katika vitendo vya wizi kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Amesema kuwa wanachama pamoja na watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo vya wizi kwa mfuko watatakiwa kurejesha fedha zote walizosababishia hasara NHIF pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria chini ya vyombo vya dola.

Dkt. Mollel amesema kuwa tusipokuwa matumizi mazuri na kuwa na uadilifu ndani ya mfuko wa bima ya afya huku ubadhirifu ukiendelea, adhma ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ya kuwa na mfuko imara wa bima ya afya kwa wote hapa nchibi hatutoifikia.

"Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Shilingi Bilioni 148 kwa ajili ya mfuko wa bima ya afya kwenda kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo kuwa na uhakika wa bima, sisi tunaosimamia mifumo, tusiposimamia kuondoa uchafu na ubadhirifu wote mfuko huu utakufa" amefafanua Dkt. Godwin Mollel.

Aidha Dkt. Mollel amesema kuwa wataenda kuchunguza pia watumishi wa afya katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF na endapo watabainika kujihusisha na vitendo hivyo vya ubadhirifu hatua kali za kisheria zitatumika dhidi yao.

Awali akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kigaigai amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na NHIF pamoja na vyombo vya usalama umebaini ubadhirifu wa shilingi milioni 520 uliosababishwa na vituo 12 vya kutolea huduma za afya, watumishi wa aya kutoka hospitali 38 na wanachama 6 wa mfuko huo.

"Ubadhirifu huu haukubaliki, natoa maelekezo kwa vyombo vya usalama wachukue hatua za haraka sana kuhakikisha kwamba fedha hizo zinarejeshwa na kuchukuliwa hatua za kisheria" amesema Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai.