Vurugu zimeenea mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini kufuatia kifungo cha rais wa zamani wa taifa hilo Jacob Zuma. 

Maduka mjini humo yaliporwa usiku kucha huku sehemu ya barabara kuu ya M2 ikifungwa. 

Ghasia hizo awali zilitokea katika mkoa wa Kwazulu Natal anapotokea Zuma siku ya Jumatano usiku wakati alipoanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 gerezani kwa kukiuka maagizo ya mahakama. 

Polisi inasema kuwa wahalifu wanatumia ghadhabu ya hatua hiyo kuiba na kusababisha uharibifu.

Shirika la ujasusi wa kitaifa NatJOINTS limeonya wale wanaochochea ghasia kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.Katika taarifa, shirika hilo la NatJOINTS limesema kuwa watu 62 wamekamatwa katika mkoa wa Kwazulu Natal na Gauteng tangu ghasia hizo kuanza.