Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) imeongeza mwito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kulinda na kusaidia raia wa Tigray.

EHRC imesema ina wasiwasi juu ya kukatwa kwa umeme, mawasiliano ya simu na huduma za maji katika maeneo kadhaa ya mkoa wa Tigray na kuongeza kuwa hali hiyo inatia doa maisha katika mkoa huo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuharibiwa kwa miundo mbinu ya umma haikubaliwi kabisa, huku Kaimu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Usaidizi wa Dharura Ramesh Rajasingham akisema zaidi ya watu laki 400,000 wameathirika na baa la njaa na wengine milioni 1.8 wako kwenye ukingo wa njaa.

Rajasingham amesema raia wanaathirika zaidi katika mzozo huo, unaosababisha mauaji, ubakaji na watu kulazimishwa kuyakimbia makaazi yao.