Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imeonesha kuwa janga la Covid-19 limesababisha ongezeko la asilimia 18 ya idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa.

Ripoti hiyo imesema hali hiyo inarudisha nyuma juhudi za kufikia lengo la kumaliza kabisa njaa duniani ifikapo mwaka 2030.

Ingawa athari kamili ya janga la ugonjwa wa Covid-19 haiwezi kubainika mara moja, ripoti ya Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa watu wapatao milioni 118 walikabiliwa na njaa mwaka 2020, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 la watu waliokabiliwa na njaa mwaka 2019.

Kulingana na ripoti hiyo, mtu mmoja kati ya kumi alikuwa na utapiamlo. Ongezeko la njaa limetokana na athari za kiuchumi katika nchi zenye kipato cha chini au kadri.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa nchi zilizoathirika zaidi na njaa ni zile zilizoshuhudia athari za mabadiliko ya tabia nchi au machafuko.