Baraza la mawaziri la Ujerumani limeidhinisha euro milioni 400 kama msaada wa dharura kwa waathirika wa mafuriko ya wiki iliyopita. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kujenga upya majengo na miundombinu ya manispaa iliyoharibiwa vibaya. 

Baada ya mkutano wa Kansela Angela Merkel na baraza la mawaziri, Waziri wa Fedha, Olaf Scholz amesema msaada huo nusu umetolewa na serikali ya shirikisho na nusu umetolewa na serikali za majimbo. 

Viongozi wa majimbo mawili yaliyoathirika na mafuriko hayo wanawajibika kutoa maelezo ya wanaopaswa kupokea msaada na kiasi gani wanapaswa kupewa. 

Kutokana na maafa hayo ambayo yamesababisha zaidi ya vifo 170 nchini Ujerumani, Scholz na Kansela Merkel wameahidi utoaji wa haraka wa msaada wa kifedha. 

Huku Ujerumani bado ikiwa inatathmini uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo, inaaminika kuwa ukarabati wa barabara na reli utagharimu takriban euro bilioni mbili.