Serikali ya Uingereza imetangaza kuanzia kuondoa masharti yote ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona. 

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na wanasayansi na vyama vya upinzani wakisema kuwa itaiweka nchi hatarini. Kuanzia saa sita ya usiku vilabu vya starehe vyote viliruhusiwa kufunguliwa tena. 

Aidha hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kama kuvaa barakoa, kuweka umbali wa mita moja na nusu baina ya watu na kufanya kazi kutoka nyumbani zote zimefutwa. 

Waziri Mkuu Boris Johnson ameutetea uamuzi wa serikali yake na kusema: "Ikiwa hatutafanya sasa, basi tutakuja kufunguwa miezi ya msimu wa baridi wakati virusi vitakapokuwa vinasambaa kwa kasi zaidi. 

Wakati huo huo tunapoteza muda wa mapumziko ambapo watoto wa shule pia wako likizo. Tunapaswa kujiuliza kama sio sasa, tutafanya lini?" Licha ya kuondolewa vikwazo, Johnson amewataka wananchi wa Uingereza kuendelea kuwa waangalifu.