Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson anatarajiwa leo kutangaza hatua ya kuondoa vizuizi vya kudhibiti kusambaa virusi vya Corona, vya uvaaji wa lazima wa barakoa pamoja na kukaa umbali wa mita kadhaa.

Vizuizi hivyo vitaondolewa katika kipindi cha wiki mbili zijazo licha ya kiwango cha maambukizo ya virusi hivyo kuongezeka kutokana na kusambaa kwa aina mpya ya kirusi cha Delta. 

Waziri mkuu huyo wa Uingereza amesema ataweka wazi kuhusu namna ya nchi hiyo itakavyoweza kujifunza kuishi na virusi hivyo. Hatua hiyo ya Johnson ni tafauti kabisa na mtazamo aliokuwa nao mwanzoni wa kuitazama Covid-19 kama adui anayetakiwa kuangamizwa. 

Kiongozi huyo wa Uingereza ameashiria kwamba hatua za lazima za kudhibiti kusambaa virusi vya Corona zitaondolewa na watu watakuwa na khiari ya kufuata wanachotaka baada ya Julai 19,siku ambayo vyombo vya habari vya msimamo mkali vimeipa jina kuwa siku ya uhuru.