Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Umoja wa  Falme za Kiarabu (U.A.E) Sheikh Shakhboot Bin Nahyan Al Nahyan Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Sheikh Al Nahyan amemshukuru Rais Samia kwa kuendeleza ushirikiano na Nchi za Falme za Kiarabu na kumkabidhi barua yenye ujumbe maalum kutoka kwa Mfalme wa U.A.E  Sheikh Mohamed Bin Zayed Al Nahyan ambapo pia mfalme huyo ametoa salamu za pole kwa Rais Samia kufuatia kifo cha Hayati Rais Magufuli na kumpongeza kwa kushika nafasi ya uongozi wa nchi.

Amesema U.A.E itaendeleza ushirikiano na uhusiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuunga mkono usawa wa kijinsia na haki za wanawake hasa wakizingatia kuwa Rais Samia ni mfano bora kwa wanawake nchini Tanzania na dunia kwa ujumla.

Aidha, Sheikh Nahyan amesema U.A.E inaunga mkono jitihada za Rais Samia za kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo amesema Umoja wa Falme za Kiarabu upo tayari kuipatia Tanzania chanjo ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Rais Samia ameshukuru Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania na kumuahidi Mjumbe huyo Maalum kuwa Serikali itaendeleza mahusiano mazuri kwa ajili ya  manufaa ya nchi hizi mbili.

Rais Samia amesema U.A.E ni mbia muhimu katika maendeleo ya Tanzania kwasababu wamesaidia kuboresha miundombinu hususan ya barabara  na biashara.

Aidha, Rais Samia  amesema kumekuwa na ongezeko la usawa wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili mwaka hadi mwaka na kuongeza kuwa Tanzania inaendelea kufanya maboresho ya kibiashara ili kuvutia zaidi wawekezaji.

Pia Rais ameshukuru kupokea mualiko wa kuhudhuria maonesho ya biashara ya kimataifa ya Dubai (Dubai Expo) yanayotarajiwa kufanyika mwezi Machi, 2022.