Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Julai 30, 2021 anatarajiwa kupokea ndege mpya aina ya Bombardier Dash 8-Q400, hafla itakayofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Kupokelewa kwa ndege hiyo kutafanya idadi ya ndege ambazo tayari zimefika nchini kuwa tisa, kati ya ndege 11 ambazo serikali imenunua.

Ndege nane ambazo tayari zimepokelewa nchini ni ndege nne aina ya Bombardier Dash 8 Q-400 (zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja), Ndege mbili aina ya Boeing 787 – 800 Dreamliner (zenye uwezo wa kubeba watu 262 kila moja) na ndege mbili aina ya Airbus A220-300 (zenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja).

Sababu kuu zilizochochea serikali kufufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ni kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa, kwani Tanzania imejijengea sifa kemukemu duniani hivyo ilikuwa aibu kutokuwa na ndege.

Pili, ni kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kuyafikia masoko ya kimataifa kwa urahisi.

Sababu ya tatu ni kukuza sekta ya utalii ambapo licha ya Tanzania kuwa ya pili kwa vivutio vingi vya utalii duniani, bado idadi ya watalii wanaoitembelea sio wengi kutokana na uwezo mdogo wa kusafirisha watalii.