Na Mwandishi wetu, Dar
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeelekezwa kushirikiana na Balozi za Tanzania katika kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji hapa nchini.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab wakati alipotembelea Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

“…………….Balozi zetu zina uhusiano wa karibu na TanTrade ambapo TanTrade moja kati ya majukumu yake ni kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wetu hapa nchini wanapata taarifa sahihi ili kusaidia kujua ni bidhaa gani za Tanzania zinaweza kuuzwa nje kwa urahisi lakini pia kujua ni nchi husika yenye uhitaji wa bidhaa hizo,” amesema Balozi Fatma

Balozi Fatma ameongeza kuwa ili bidhaa za Tanzania ziendelee kuuzwa katika masoko ya kimataifa ulimwenguni, TanTrade iendelee kushirikiana kwa karibu na Balozi za Tanzania katika kuhakikisha kuwa inatoa taarifa sahihi za bidhaa.

“Ushirikiano baina ya TanTrade na Balozi zetu uendelee kuimarishwa ili kuwawezesha wafanyabiashara kupata taarifa sahihi na kwa wakati, lakini pia ushirikiano huu utasaidia kutangaza fursa za biashara zilizopo nchini Tanzania katika Mataifa ya Kigeni,” amesema Balozi Fatma

Balozi Fatma pia ametoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya maonesho ya Sabasaba kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ya Nchi walioshiriki katika maonesho hayo ili kujua ni kwa namna gani wataweza kunufaika na fursa za kuuza bidhaa zetu kwenye nchi za kimataifa

“Kupitia maonesho haya watanzania watumie fursa hii kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ya Nchi walioshiriki katika maonesho haya, lakini pia kuangalia ni namna gani watanufaika na fursa za kuuza bidhaa zetu kwenye nchi za kimataifa,” Amesema Balozi Fatma Rajab.