Julai 30, 2021 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) iliungana na wadau wote ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kupinga Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu Duniani. Siku hii ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Novemba 15, 2000 kupitia Azimio Na. 55/25, na ilianza kuadhimishwa rasmi Julai 30, 2003.

Lengo la kuwepo kwa siku hii, pamoja na mambo mengine, ni kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ukatili na unyonyaji unaotokana na biashara hii.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya kimataifa ni: “Tuwasikilize Wahanga, tujifunze kutoka kwao juu ya kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu” (Victims’ voices lead the way), ikiangazia nafasi ya wahanga katika jitihada za kukomesha biashara hii haramu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokumbwa na tatizo la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, ambapo waathirika wakubwa ni vijana, wanawake, wasichana na watoto. Watu hawa hutolewa vijijini, hususan vijiji maskini baada ya kudanganywa na kupatiwa fedha kidogo, wao wenyewe, ama familia zao, na mara nyingine nguvu hutumika ili kuwapata.

Wahanga wa biashara hii awali hupewa ahadi za kimaslahi, lakini kiuhalisia hufanyishwa kazi zenye ukandamizaji, unyanyasaji na ukatili na hata kutolewa baadhi ya viungo vyao vya mwili na kuuzwa. Kwa ujumla vitendo wanavyofanyiwa ni kinyume na mikataba ya kimataifa, kikanda na sheria za nchi. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu Uliopangwa Kimataifa (United Nations Convention Against Transnational Organized Crime, 2000); Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (1966); Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (1966); Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989); Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (1981) na mingine mingi ambayo Tanzania imeridhia.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 zinatamka bayana kuwa binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa; hivyo, kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru na anayo haki ya kufanya kazi na kupata ujira unaolingana na kazi yake.

Kutokana na kushamiri kwa biashara hii haramu na ili kukidhi matakwa ya mikataba ya kimataifa inayosimamia mapambano dhidi ya biashara hii, Tanzania ilitunga Sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu (Na. 6 ya mwaka 2008). Chini ya Sheria hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeunda Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu na Sekretarieti ili kusimamia utekelezaji wake na kuunganisha nguvu kutoka kwa wadau mbalimbali ili kupambana na biashara hiyo.

Pia, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inatekeleza Mpango Kazi wa miaka mitatu mitatu wenye dira ya kuifanya nchi iondokane kabisa na biashara haramu ya binadamu na kutoa huduma bora kwa wahanga wa biashara hiyo.

Vile vile Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetunga sheria mbili zinazolinda ustawi wa mtoto – Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 (upande wa bara) na Sheria ya Mtoto Na. 6 ya mwaka 2011 (upande wa Zanzibar). Aidha,  Serikali imeongeza kipengele kinachotafsiri na kutoa adhabu kali dhidi ya watu wanaofanya biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu katika Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 rejeo la 2016. Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wadau wengine wana majukumu ya kipekee katika kutekeleza sheria hii, ikiwa ni pamoja na kuchunguza makosa, kutambua, kulinda na kusaidia waathirika pamoja na kuwahoji watuhumiwa wa makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kuchukua fursa hii kuzipongeza kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wengine kwa juhudi za kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu inayofanyika ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa.

Kwa lengo la kulinda na kuheshimu haki za binadamu, Tume inapendekeza yafuatayo:

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu iongeze jitihada za utoaji elimu kwa umma ili kukomesha biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

    Serikali kupitia taasisi zake zinazopambana na usafirishaji haramu wa binadamu zianzishe mfumo wa utoaji huduma muhimu kwa wahanga ili kuhakikisha kuwa wanarejea katika hali zao za kawaida na kuwaunganisha na familia zao.

    Wazazi na walezi wajitahidi kupata taarifa za kutosha kabla ya kukubali watoto wao kuchukuliwa na kupelekwa kufanya kazi ndani na nje ya nchi.

Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wote katika kuhakikisha kuwa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu inakomeshwa na haki za binadamu zinaheshimiwa na kulindwa na kila mmoja wetu.