Kundi la Taliban limeanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa mkoa nchini Afghanistan, ya kwanza tangu Marekani ilipoanza kuondoa wanajeshi wake nchini humo, katika muendelezo wa mashambulizi makali ya waasi hao. 

Mapigano makali yamezuka katika mji wa magharibi wa Qala-i-Naw, ambao ndiyo mji mkuu wa mkoa wa Badghis, ambap wapiganaji wa Taliban wamefanikiwa kudhibiti makao makuu ya polisi pamoja na ofisi za idara ya taifa ya upelelezi. 

Waziri wa ulinzi wa Afghanistan Bismillah Mohammadi, amesema vikosi vilikuwa katika hali nzito ya kijeshi, na kuongeza kuwa vita vilikuwa vimepamba moto na Wataliban. 

Mashambulizi haya yamejiri saa chache tu baada ya Marekani kutangaza kuwa vikosi vyake nchini humo vimekamilisha asilimia 90 ya mchakato wa kuondoka kutoka Afghanistan, huku serikali ya Kabul akifanya mazungumzo na wawakilishi wa Taliban katika taifa jirani la Iran.