Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imekutana katika kikao maalumu Alhamisi 29 Julai, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan.

Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuruhusu chanjo ya virusi vya ugonjwa wa korona (UVIKO 19) Kutolewa nchini na yeye kuwa mfano wa  kukubali kuchanjwa ikiwa ni udhibitisho wa usalama wa chanjo hiyo.

Uamuzi wake umetajwa kuwa ni kielelezo cha upendo na uzalendo mkubwa alionao katika kujali afya za watanzania na ni hatua nzuri ya Tanzania kuungana na dunia katika kukabiliana dhidi ya UVIKO-19, pia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025 Ibara ya 83(o) na 84.

Kamati Kuu imeelekeza kuanza kuchukuliwa hatua kwa wale wote wanaokiuka mienendo, taratibu na kanuni za maadili na uongozi kwa mujibu wa katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Aidha Kamati Kuu imefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi ambapo Ndugu Gilbert Kalima Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania na Dkt. Philis Nyimbi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania  (UWT).

Shaka Hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Itikadi na Uenezi
29 Julai, 2021.