Maafisa wa Shirika la Afya Duniani WHO wamesema hakuna ushahidi wa kutosha unaonyesha kwamba watu wanahitaji kuchomwa sindano ya tatu ya chanjo dhidi ya virusi vya corona, na hivyo kutoa wito wa chanjo zilizobakia kupewa mataifa maskini ambayo bado hayakuchanja raia wake, badala ya kutumiwa na nchi tajiri kama nyongeza.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari, mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema utofauti katika kusambaza chanjo duniani umetokana na kile alichokiita "tamaa", na kuyataka makampuni yanayotengeneza chanjo kuzipa kipaumbele nchi maskini.
Ghebreyesus amezitolea wito kampuni za chanjo ya Pfizer na Moderna kuusaidia mpango wa Umoja wa Mataifa wa ugavi wa chanjo ulimwenguni "COVAX”, Timu ya Kusambaza Chanjo Afrika, na nchi nyingine za kipato cha chini na cha wastani.