Sheria Zilizopitwa Na Wakati Yatajwa Chanzo Cha Halmashauri Kuwa Na Uhafifu Wa Ukusanyaji Mapato.
Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Sheria ndogondogo zilizopitwa na wakati imetajwa kuwa ni chanzo cha halmashauri nyingi hapa nchini kuwa na uhafifu wa ukusanyaji wa mapato hali ambayo husababisha halmashauri hizo kudorora na kushindwa kujiendesha.
Hayo yamebainishwa Julai 14,2021 ,jijini Dodoma na Mtaalam Mshauri wa Mradi wa Program ya kuboresha mifumo ya fedha za umma unaoratibiwa na shirika la Maendeleo la Ujerumani [GIZ] Raymond Nzali wakati akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo kwa halmashauri mbili za jiji la Dodoma na Halmashauri ya Chamwino.
Amesema ni muhimu kupitia sheria ndogondogo ili kwendana na wakati wa sasa hali ambayo itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato pamoja na kubuni mbinu mpya za ukusanyaji mapato kwendana na wakati wa sasa.
Akizindua mafunzo ya mradi huo kwa viongozi wa halmashauri,Katibu tawala mkoa wa Dodoma Bi.Fatma Mganga amesema chanzo cha jiji la Dodoma kuanza kushuka ukusanyaji wa mapato kutoka bilioni 72 hadi nusu yake ni kutokana na utegemezi wa chanzo kimoja tu cha mapato ambacho ni ardhi hivyo kuna haja ya kuongeza nguvu kuangalia vyanzo vingine.
Katibu tawala huyo amesema baada ya mafunzo hayo kwa viongozi wa halmashauri itasaidia kuwajengea uwezo kwa kuongeza vyanzo vingine vya ukusanyaji mapato.
Mradi wa Program ya kuboresha mifumo ya fedha za umma ulianza Mei,2016 ukiwa na halmashauri 15 ambapo sasa awamu hii ya pili upo katika halmashauri 21 na mikoa 7 ya Dodoma ,Singida,Pwani,Arusha,Tanga,Kigoma na Mwanza .