Na. Beatrice Sanga-Maelezo
Jumuiya ya kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wametoa Dola za Kimarekani milioni 6 kwa ajili ya kufanyika upembuzi  yakinifu wa ujenzi  wa reli ya kimataifa ya Mtwara mpaka Mbambabay ambayo inategemewa kufungua fursa nyingi kwa wananchi wa Mtwara na kanda ya Kusini

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha mkutano wa SADC ambao unahusisha mawaziri wa fedha na uwekezaji wa nchi wanachama wa jumuiya ya SADC uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Akieleza mambo ambayo yanaendelea kujadiliwa na mafanikio ambayo yamefikiwa kutokana na kikao hicho Waziri jamal Kassim ali amesema kikao hicho kimepata fursa ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu sera ya kifedha , za kikodi pamoja na uwekezaji na biashara katika Kanda ya Jumuiya ya SADC ambapo pamoja na hayo fedha zilizotolewa na SADC zinaenda kusaidia upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli hiyo ya Mtwara-Mbambabay ambayo itaenda kufungua uchumi wa Mtwara na kanda nzima ya kusini

“jambo kubwa ambalo ningependa mjue ni kwamba katika mwendelezo wa vikao hivi wenzetu wa SADC wameweza kutupatia takribani Dola milioni 6 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya Mtwara mpaka Mbambabay ambayo itajengwa ili kurahisisha na kuifungua Mtwara na kanda hii ya kusini kiuchumi na mpaka sasa tayari SADC wametupatia pesa hizo” amesema Mh. Jamal Kassim Ali

Mh. Jamal Kassim Ali, ameongeza kuwa  katika vikao vilivyopita mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo wa nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC wenye lengo la kuchochea maendeleo katika nchi wanachama  na kuzitaka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya SADC  kushikana mikono kuhakikisha kwamba mfuko huu muhimu unaanzishwa

“ sisi kama Tanzania kama ambavyo tumekuwa vinara katika kuhakikisha masuala ya ukombozi wa SADC  kisiasa, sasa tunakwenda na ajenda hii tuwe vinara katika ukombozi wa kisiasa lakini pia ukombozi wa kiuchumi. Tunaomba nchi zote wanachama wa Jumuiya ya SADC kwa umuhimu ambao mfuko huu utakuwa katika uchumi wa nchi zetu kuna haja kama nchi zote wanachama wa jumuiya ya SADC tushikane kuhakikisha kwamba chombo hiki muhimu tunakianzisha” amesema Mhe. Jamal Kassim Ali

Aidha ameongeza kuwa kutokana na changamoto ya ugonjwa wa uviko 19 (COVID  19) uchumi wa nchi nyingi ikiwemo Tanzania umeathirika hivyo kupitia vikao hivyo hoja mbalimbali zitafikishwa kupitia jukwaa hilo la SADC kama chombo cha kikanda kuweza kueleza namna gani tunaweza tukasimama pamoja kupeleka sauti zetu na kusema zile changamoto zetu ambazo ni kodi na masharti yaliyotokana na makubaliano yaliyokuwepo.

“ kwa bahati nzuri wenzetu waAfrika Kusini wao ni wanachama katika jumuiya ya G20 ambayo inahusisha nchi nyingi ambazo zinatusaidia kwahiyo kupitia wao tunataka kupeleka ujumbe wetu kwamba katika maeneo muhimu tunaona ipo haja yale mambo au masharti ambayo yamewekwa yatizamwe upya ikiwemo swala la utozaji wa kodi na kuongezeka kwa riba na masharti mengineyo yanayohusu uratibu wa malipo , kwa hiyo kupitisa jukwaa hili la SADC  tutapeleka hii hoja kupitia wenzetu Afrika Kusini ambao ndo nchi pekee kutoka SADC wanaoingia wakapaze sauti hii” amesema Mhe. Jamal Kassim Ali