Rais Samia  amezungumzia suala la misamaha ya kodi hasa katika taasisi za dini akieleza kuwa wakati mwingine serikali inalazimika kutoka kodi kwenye elimu na afya zinazoendeshwa na taasisi hizo kwa vile baadhi zimeonekana kama ni za kibiashara zaidi na si utoaji wa huduma.

Aidha, amesema serikali inakwenda kuangalia mfumo wote wa kodi nchini ikihusanisha na ukuaji wa uchumi, maoteo ya ukuaji wa uchumi na kuona kodi ambazo zinaweza kufutwa, kupunguzwa ama kuzisamehe.

Rais Samia alisema hayo jana katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) uliofanyika mjini Morogoro.

Katika hatua hiyo, Rais Samia alisema serikali imeanza kufanya mapitio ya kodi na kuzifuta ikiwemo sheria ya fedha ambayo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, imefuta tozo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi ambayo ilikuwa inalalamikiwa na taasisi za dini kwenye suala la elimu.

Alisema suala hilo litakapokamilika kuna uhakika ya kwamba mambo mengi yanayolalamikiwa na taasisi za dini yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.

Alisema wakati mwingine serikali inalazimika kutoka kodi kwenye elimu na afya zinazoendeshwa na taasisi za dini kwa vile baadhi zimeonekana kama ni za kibiashara zaidi na si utoaji wa huduma.

Rais Samia alisema suluhisho la hilo ni kwamba wote wafanye kazi kwa uwazi na kuaminiana. “Ninaposema kufanya kazi kwa uwazi ni kwamba mamlaka za kodi wakati wa ukaguzi wake kuwepo na uwazi wa mahesabu…niombe sana tufanye kazi kwa uwazi na kuaminiana,” alisisitiza.

Alisema huduma za elimu na afya pia zinatolewa na taasisi binafsi na viwango vyake vya gharama zinazotozwa na taasisi za dini hazitofautiani na za taasisi binafsi hivyo kuonekana nazo zinafanya biashara.

“Endapo tutaondoa kodi kwa taasisi za dini ambazo shughuli zao zinafanana kama zile za sekta binafsi hakutakuwa na usawa wa kibiashara za ushindani hivyo suala hili linapaswa kuangaliwa kwa mapana ili usiathiri upande mwingine,” alisisitiza Rais Samia.