Rais Samia  amewaomba viongozi wa dini nchini kuwa ni sehemu ya kutoa elimu kwa waumini wao juu ya umuhimu wa sensa katika mipango ya maendeleo wakati nchi inapoanza maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti mwakani.

Aliyasema hayo jana katika hotuba yake mjini hapa ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

“Agosti mwaka 2022 nchi yetu ina zoezi la sensa la kuhesabiana ili kujua Watanzania idadi yetu tupo ngapi, ni zoezi muhimu sana kwa maendeleo yetu, takwimu ya idadi ya watu inasaidia taifa kupanga maendeleo yake,” alisema Rais Samia.

Alisema kazi hiyo ni muhimu kwani kuwepo kwa takwimu ya idadi ya watu (watoto, vijana na watu wazima)  kunawezesha serikali kutambua mahitaji na malengo yake ili kuweka mipango ya maendeleo na ufuatiliaji wake.

“Bila takwimu nzuri basi mipango yote ya maendeleo ni kama mnabahatisha tu hamwendi vizuri…mkiwa na takwimu sahihi basi mipango ya maendeleo inakwenda vizuri,” alibainisha Rais Samia.

Aliwaomba viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kushiriki kutoa elimu kwa wananchi wao (waumini) ili kuwaondolea dhana ya imani potofu inayoweza kujitokeza kuhusiana na sensa ya watu.

“Sensa si suala geni kwetu hapa kwani imeandikiwa katika kila kwenye vitabu vya dini zetu hivyo viongozi wa dini wanao wajibu pia wakusaidia kutoa elimu,” alisema Rais Samia na kuongeza kuwa serikali ipo bega kwa bega na viongozi wa dini na suala lolote la ushauri kwa serikali milango ipo wazi kwao.