Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inayashughulia malalamiko yote yanayotolewa na Watanzania kuhusu tozo mpya za miamala ya simu zilizoanza kutumika Jula 15 mwaka huu.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, hii leo Julai 19, 2021, akitoa tammko la serikali akiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile na kuwaomba Watanzania kuwa watulivu kwani serikali inafanyia kazi malalamiko yote.

“Tayari Mheshimiwa Rais ameshaguswa na jambo hili amesikia maoni ya Watanzania wote na amesema tuyafanyie kazi jambo hili.

“Kwa hiyo,nitoe rai kwa wananchi kuwa Serikali imesikia malalamiko ya wananchi na tayari tumeendelea kuyafanyia kazi, Waziri Mkuu ameshaitisha kikao kesho kuendelea kupitia masuala haya haya.


“Nitoe rai kwa wananchi kuwa watulivu kwenye jambo hili, tutaendelea kufafanua kwenye maeneo ambayo yanahitaji ufafanuzi na tutachukua hatua kwenye maeneo ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua "Amesema Waziri Nchema.

Huku akitaka sheria ziheshimiwe, Waziri Mwigulu ameonya watu wanaopotosha jambo hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu.

“Nitoe rai kwa ambao wanapenda kupotosha au kubadili dhana ya jambo ambalo limekusudiwa na lina maslahi mapana ya Taifa letu wasifanye hivyo. Sheria za nchi zinapaswa ziheshimiwe, hakuna haja ya kuwasikiliza wapotoshaji."

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile amesema; “Niwasihi Watanzania tuwe watulivu wakati jambo hili linafanyiwa kazi, Serikali yetu ni sikivu, na itaenda kulifanyia kazi jambo hili kuhakikisha tunafikia mwafaka mzuri"