Polisi nchini Haiti imesema imemkamata Raia wa Nchi hiyo aliyetumia ndege binafsi kushirikiana na Watu wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji ya Rais wa Haiti, Jovenel Moise.

Mkuu wa Polisi wa Haiti, Leon Charles amesema Mtuhumiwa huyo anaitwa Christian Emmanuel Sanon, mwenye umri wa miaka 63 anayeishi Florida, Marekani.

Amesema Sanon alikwenda Haiti kwa kutumia ndege binafsi mwanzoni mwa mwezi Juni akiwa na Walinzi binafsi na alitaka kuchukua nafasi ya Urais.

Sponsored: Nafasi Mpya za Kazi Tanzania, Bofya Hapa

Mkuu huyo wa Polisi hakueleza nia ya Sanon, zaidi ya kusema zilikuwa kisiasa na kwamba aliwasiliana na Mtuhumiwa mmoja baada ya kukamatwa, Charles amewaambia waandishi habari kwamba nia ya washambuliaji hao awali ilikuwa kuhakikisha usalama wa Sanon, lakini baadae lengo lilibadilishwa na walimpa mmoja wa Wauaji hati ya kumkamata Rais na kwamba Polisi walipata vitu kadhaa kwenye nyumba ya Sanon.

”Ndani ya nyumba ya Sanon, tumepata kofia yenye nembo ya Mamlaka ya Kupambana na Biashara Haramu ya Madawa nchini Marekani, DEA, masanduku sita ya kuwekea bunduki, maboksi 20 yenye risasi, vibao vinne vyenye namba za magari zilizosajiliwa kwa namba za Jamhuri ya Dominika, magari mawili na mawasiliano aliyofanya na watu wasiojulikana”Charles.

Charles amesema jumla ya Raia 26 wa Colombia wanatuhumiwa kumuua Rais Moise Jumatano iliyopita, 18 kati yao wamekamatwa pamoja na Raia wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani, amesema bado wanaendelea kuwasaka Watuhumiwa watano na kwamba Watuhumiwa watatu wameuawa.