Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametoa wito wa kuwepo amani na mazungumzo kufanyika nchini Cuba, baada maandamano yasiyo ya kawaida kulikumba taifa hilo la kikomunisti. 

Akizungumza katika hotuba zake za kila wiki, kwenye uwanja wa Mtakatifu Peter, Papa Francis amesema yuko pamoja na watu wa Cuba katika nyakati hizi ngumu. 

Papa amezungumza kwa mara ya kwanza katika uwanja huo, tangu aliporejea Vatican baada ya kulazwa hospitali kwa siku 11 baada ya kufanyiwa upasuaji. 

Papa pia ametoa wito wa kumalizika ghasia Afrika Kusini na pia ameyataja mafuriko yaliyosababisha vifo nchini Ujerumani, Ubelgiji na Uholanzi kuwa maafa.