Ofisi ya Waziri Mkuu, imetembelea na kukagua kasi ya utekelezaji wa miradi ya Afya inayohusisha ujenzi majengo pamoja na  mifumo ya utoaji huduma  za afya kwa wananchi, inayofadhiliwa na serikali pamoja  na Mfuko wa Dunia -Global Fund katika mikoa ya Tanga na  Killimanjaro na kuagiza miradi yote iliyosimama ujenzi ikamilike haraka iweze kutoa huduma kwa wananchi 


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Bw. Kaspar Kaspar Mmuya alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya ukaguzi miradi hivi karibuni na kubaini kuwapo changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizosababisha miradi kuchelewa na kushindwa kukamilika kwa wakati hadi kusimama ujenzi. Aliwataka watendaji wote wanaohusika katika ujenzi wa miradi hiyo kufuatilia haraka na kwa karibu changamoto zote zilizojitokeza katika utekelezaji miradi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kuwezesha miradi kukamilika na kuanza kazi

Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo Mratibu wa utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi na utoaji huduma za afya inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia- Global Fund, inayolenga  kupambana na magonjwa ya Kifua Kikuu, UKIMWI, Malaria pamoja na kuboresha Mifumo Endelevu ya Utoaji wa Huduma za Afya. Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw.Tixon Nzunda,  
ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Kitaifa  inayoratibu Matumizi ya fedha zinazotolewa na mfuko wa Dunia.

Hivyo, katika ziara hiyo ya ukaguzi ya siku tano, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alimuwakilisha Katibu Mkuu na aliambatana na  timu ya Wataalam kutoka Ofisi yake ya  Waziri Mkuu; Ofisi ya Rais TAMISEMI; Wizara ya Afya, ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; na Sekretarieti ya Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ya Global Fund ambao walitembelea mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kwa lengo la  kubaini kiini cha changamoto zilizopo zinazosababisha miradi kukwama ujenzi
 
Miradi iliyotembelewa, kukaguliwa na kutolewa maagizo na Naibu Katibu Mkuu Mmuya katika awamu hii ya kwanza akiwa na timu yake ya wataalamu ni pamoja na  ujenzi  ni jengo la ghorofa moja  la Wazazi (Mama na Mtoto) katika hospitali ya halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, na majengo mawili yanayojengwa  katika hospitali ya  ya rufaa ya mkoa- Mawezi, mkoani Kilimanjaro moja likiwa la kawaida litakalotoa huduma za dharura (Emergency Medicine Department-EMD) na jengo la ghorofa nne la Mama na Mtoto  (Martenity Block)  

Wakati wa zoezi la ukaguzi watendaji katika miradi hiyo, kwa wakati tofauti, walimueleza Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake kuwa miradi hiyo ya ujenzi pamoja na uboreshaji wa mifumo endelevu ya utoaji wa huduma za afya kwa umma haijakamilika kwa wakati kutokana na changamoto za kiutendaji katika kutekeleza majukumu ikiwa ni pamoja na kuchelelewa vibali vya kuruhusu kupata fedha kuweza kuikamilisha miradi kwa wakati. Miradi yote aliyotembelea na kuikagua Naibu Katibu Mkuu Mmuya kama mratibu, akiwa na wataalamu wake aliishuhudia ikiwa haijakamilika kwa muda uliopangwa na imesimama ujenzi.

Akiongea baada ya ukaguzi wa Miradi Naibu katibu Mkuu Mmuya aliwapongeza watendaji kwa namna walivyoweza kusimamia uwepo wa miradi hiyo na kufikia hatua ilivyo na kuwahimiza kuendelea kuisimamia huku wakifuatilia kwa kasi  ufumbuzi kwa changamoto zilizopo na kuhakikisha miradi inakamilika na kuanza  kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

“Nawapongeza watendaji wote katika miradi hii kwa jitihada zenu kuhakikisha miradi hii inakuwepo na inafikia hatua hizi nzuri katika ujenzi. Miradi hii ni ya lazima na muhimu sana kwa wananchi, hivyo haina budi kusimamiwa kwa weledi na ufanisi na kutatua changamoto zinazojitokeza kukwamisha miradi kukamilika kwa wakati na kuifanya isiweze kutoa huduma kwa wananchi” alisema Naibu Katibu Mkuu Kaspar Mmuya na kuongeza kuwa: “Ofisi ya Waziri Mkuu kama Mratibu imedhamiria kufuatilia na kuratibu kwa ufaisi miradi hii ya ujenzi katika sekta ya afya yenye ufadhiliwa wa pamoja na Mfuko wa Dunia iweze kuleta tija”

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Kaimu Mganga Mkuu Dkt.  Gasto Stephen  alitoa taarifa  kwa Naibu Katibu Mkuu Mmuya   kuhusu maendeleo  ya  ujenzi wa jengo la ghoofa  la ‘Mama na Mtoto’ akisema jengo hilo  halijakamilika na limesimama  ujenzi  kwa sasa. Alisema lilianza kujengwa Juni 1, 2020 na lilipaswa kukamilika, Marchi 1, 2021. Aidha alisema Mfuko wa Dunia -Global Fund   ulitoa  shilingi  za kitanzania 400,000.000/- mwezi Mei mwaka 2019 kukamilisha ujenzi na jengo hilo  ambalo  likikamilika litaweza kutoa huduma  za upasuaji  za dharura kwa akina mama , huduma za mama wajawazito wanaosubiri kujifungua , huduma za kujifungua, huduma baada ya mama kujifungua na huduma za watoto njiti.
changamoto zilizopelekea mradi huo  kukwama  kukamilika  zilielezwakuwa ni pamoja na  mabadiliko ya ramani  ya mwanzo ya jengo  hilo la ‘Mama na Mtoto’ ambapo  lilikuwa jengo la kawaida  lakini kutokana na ufinyu na jiofrafia  ya eneo  la hospitali ya wilaya ilipendekezwa kuwa  jengo la   ghorofa ili  kupata nafasi ya kutosha  ya utoaji huduma zote  zilizotajwa.


Aidha alielezwa changamoto ya  bajeti ndogo kulingana na tathmini ya mradi,  ongezeko la gharama za ujenzi  kutokana na  mabadiliko ya bei ya vifaa  vya ujenzi,   na wazabuni wa vifaa hivyo kuwa wachache,  kutopatikana kokoto  za mashine katika eneo la Lushoto, upatikanaji wa nondo na bati kutoka kiwandani uliohitaji kusubiri kwa muda pamoja na kuwapo mvua za mara. 


Changamoto nyingine zilizoelezwa kuchelewesha jengo kukamilika ni  mchakato wa manunuzi wakati wa kuomba  ondoleo la kodi pamoja na mchango wa Halmashauri  kupitia  mapato ya ndani kuathiriwa  na mabadiliko ya Tabianchi  pamoja na ugonjwa wa unaosababishwa na virusi vya Korona (UVIKO 19) hivyo, kusababisha jengo kutokamilika kwa wakati.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lushoto Bibi Ikupa Harrison Mwasyoge  alimweleza Naibu Katibu Mkuu Kaspar  na timu yake ya wataalamu kuwa  kutokana na changamoto zilizojitokeza za ukusanyaji wa mapato ya ndani, Halmashauri yake iliomba  kuongezwa bajeti ya shilingi za kitanzania 364,907,640.1/- ili kumalizia mradi wa jengo hilo la ‘Mama na Mtoto’ ndani ya mwezi Julai, 2021.


Taarifa aliyopewa Naibu Katibu Mkuu  kuhusu fedha kwa ajili ya mradi huu iliainisha kuwa jumla ya fedha zinazohitajika  sasa kukamilisha mradi  huo wa ujenzi wa jengo la ‘Mama na Mtoto’ baada ya makadirio  mapya ni shilingi  zipatazo  810,848,342.10 ambapo fedha za ujenzi  wa jengo ni shs. 694,582.778 na fedha za vifaa tiba ni sh.116,265,564. Hadi Mwezi Mei, 2021 jumla ya matumizi ya fedha yalikuwa shs. 439,417,222  ambapo kazi ya  ujenzi imefikia asilimia 78 na muda uliotumika ni asilimia 94.


Akitoa Maagizo, Naibu Katibu Mkuu Mmuya  alimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuandika barua kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kupata majibu ya barua yake ya mwaka 2020 kuhusu maombi ya fedha za kukamilisha mradi huo na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kufanya   uchambuzi wa mahitaji halisi ya kukamilisha ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto na kuyawasilisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI ili jengo likamilike kwa wakati na kuitaka  Halmashauri pia iwasilishe maombi Ofisi ya Rais, UTUMISHI ya kujaza nafasi za wakuu wa  zinazokaimiwa ili kuongeza ufanisi katika shughuli zake. 


Mkoani Kilimanjaro, katika majumuisho ya ziara yake Naibu Katibu Mkuu aliagiza hatua za utekelezaji kutatua changamoto zilizokwamisha ujenzi wa majengo kwa kumuelekeza Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Abdallah Seif Shekalaghe kufuatilia kwa karibu na haraka upatikanaji wa kibali cha msamaha wa kodi kwa manunuzi ya vifaa vya ujenzi (GN- Government Notice) wa jengo la huduma za dharura ili kuhakikisha manunuzi yanafanyika mapema iwezekanavyo. 


“Fuatilieni haraka hiyo GN kuweza kupata msamaha wa kodi. Andaeni pia  mkakati mahsusi wa kusimamia hospitali za rufaa za mikoa na kanda badala ya kusimamiwa na Wizara ya Afya moja kwa moja”  Naibu Katibu Mkuu alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na timu yake ya wataalamu  wakati wa kikao cha majumuisho kilichofanyika  ofisi kwake.
Awali Naibu Katibu Mkuu Mmuya alikagua miradi hiyo ya ujenzi majengo katika hospitali Kongwe ya mkoa–Mawenzi, Mkoani Kilimanjaro ambapo alipewa taarifa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt Credianus Mgimba kuwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura (Emergency Medicine Department) umekwama kukamilika na kwamba changamoto zilizopo katika utelekezaji ujenzi ni pamoja na kibali cha msamaha wa kodi kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi (GN) kuchukua muda mrefu. 


Kwa mujibu wa Dkt. Mgimba, jengo hilo la  huduma za dharura likikamilika litasaidia kuboresha  huduma za dharura  pale wanapopokea wagonjwa wa dharura kwa wakati mmoja na kuweza kutoa huduma kwa wakati,  kuboresha huduma za wagonjwa mahututi, kuboresha utoaji huduma wa vipimo vya dharura pamoja na kutatua changamoto ya msongamano wa wagonjwa.  


Ujenzi wa mradi wa jengo la huduma za dharura ulianza mwezi Machi, 2020 na ulitarajia kukamilika mwezi Machi, 2021, na sasa unategemewa kukamilika ifikapo mwezi Augusti, 2021. Makadirio ya ghrama za mradi huu ni shilingi 764,995,974.  


Aidha alielezea mchanganuo  wa mapokezi na matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo hilo katika  kipindi cha utekeezaji  cha mwaka 2019/2021 kuwa   hadi sasa fedha zimepokelewa toka Global fund  kwa awamu mbili, awamu ya kwanza Tshs 262,400000(mwezi Juni 2019) na awamu ya pili zilipokelewa shilingi 514,083,631.31 (Mwezi  Disemba 2020) .Mradi umefika asilimia 84 ya utekelezaji.


Kuhusu mradi wa ujenzi jengo la ‘Mama na Mtoto’ (Martenity Block Complex), Naibu Katibu Mkuu Kaspar alielezwa kuwa changamoto zilizokwamisha ujenzi kukamilika kwa wakati ni muda mrefu kwa upatikanaji kibali cha msamaha wa kodi na suala la kutotenganisha utendaji wa majukumu ya kimkataba kama vile shughuli za fundi mkuu na mshauri elekezi zinafanywa na mtaalamu wa aina moja na kusababisha ugumu katika udhibiti ubora na uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi.


Mradi huu ukikamilika ujenzi utasaidia   kuboresha huduma za Mama na Mtoto na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto chini ya miaka  mitano. Pia jengo litasaidia  kutatua  changamoto ya msongamano wa wagonjwa  katika wodi  ya wazazi  inayotumika sasa,  kusaidia kuboresha huduma za wagonjwa wanaohitaji uangalizi  wa karibu (ICU) pamoja na kupunguza rufaa zisizo lazima kwenda hospitaliya rufaa KCMC,  kuboreshwa kwa huduma za  vipimo kama vile CT-Scan, MRI, Xray na Ultrasound kuboresha  kuduma za upasuaji ambapo zitafanyika kwa ubora na kwa wakati kutokana na uwepo wa vyumba upasuaji vya kutosha.


 Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga mkuu wa Mkoa kwa Naibu Katibu Mkuu Mmuya, Ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto ulianza mwaka wa fedha 2009/2010 na Mkandarasi binafsi ambapo mwaka 2016 alikabidhiwa kwa wakala wa Majengo-Tanzania Building Agency (TBA) kuendela na ujenzi chini ya usimamizi wa ofisi ya Katibu Tawala-(RAS) mkoa wa Kilimanjaro ambapo makadirio  ya ujenzi wote ilikuwa   shilling 10.5 bilioni .  Aidha utekelezaji wa mradi huu umefanyika kwa awamu 7 , awamu ya kwanza  hadi ya sita ulikuwa chini ya Katibu Tawala wa Mkoa na awamu ya saba  unafanyika chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na watoto ambapo katika awamu ya saba mradi umetekelezwa kwa asilimia 43 kulingana na kazi zilizofanyika  na Wakala wa majengo Tanzania(TBA).


Mchanganuo wa mapokezi na matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo  hili la Wazazi mwaka 2008/2009  hadi  2019/2020 katika hospitali kongwe ya Mawezi  ulionesha kwamba awamu ya kwanza  ya ujenzi hadi  awamu ya sita katika mwaka  2008/2009 hadi 2017/2018 chanzo cha fedha ilikuwa ruzuku kutoka serikali kuu.   Hadi sas ujenzi jengo hili la Mama na Mtoto umekamilika asilimia 70. Na tangu jengo lilipokabidhiwa wizara ya afya (awamu ya 7) ujenzi umekamilika kwa asilimia 43% ya lengo la ujenzi katika awamu hiyo.


Aidha tangu ujenzi wa mradi   wa jengo la Mama na mtoto ulipoanza mwaka 2009 hadi sasa zimetumika jumla ya shilingi Bilioni 6.4 na bado shilingi Bilion 4.1 kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa makadirio ya awali mwaka 2009.


Naibu Katibu Mkuu Mmuya alielezwa na  Dkt. Mgimbi  kuwa  katika awamu ya saba  wamepokea kiasi cha shilingi 1,778059098/- kutoka Global Fund  na fedha zilizotumika ni  sh. 1,667,637,689/- kati ya fedha hizo kiasi cha sh.550,219921.15 zimetumika kumlipa TEMESA na shilingi 172,686,326.48 zimetumika kumlipa mjenzi TBA na shilingi 944,731447 zimetumia kwa ajii ya vifaa vya ujenzi.