Na Mwandishi Wetu Dodoma
Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) limemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kukutana nao na kuzungumza kuhusu mustakabali wa NGOs kwa maendeleo ya taifa.

Haya yamesemwa leo (09/07/2021) jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) Lilian Joseph Badi wakati wa kukamilisha zoezi la uchaguzi wa viongozi wa Baraza hilo.

Lilian amesema kuwa lengo la kutaka kukutana na Rais ni kuweka muelekeo mzuri kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika jitihada za kuhakikisha yanasaidiana na Serikali kuwaletea maendeleo wananchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali .

Bi Lilian ameongeza kuwa Baraza hilo litahakikisha linaleta umoja kati ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, wadau na Serikali ili kuhakikisha inasaidia utekelezaji wa mipango mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amelitaka Baraza hilo kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria taratibu na tamaduni za nchi ili kusaidiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika kujiletea maendeleo.

Ameongeza kuwa Baraza hilo linatakiwa kuhakikisha linaweka maslahi ya taifa mbele na kuhakikisha linasimama badala ya Mashrika yote na sio kwa ajili ya Mashirika machache tu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga amelipongeza Baraza hilo kwa kuchagua viongozi wake na kuwataka kuwa jicho kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.

Hivi karibuni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima aliunda Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) ambao umekamilika kwa kuchagua viongozi wa Baraza hili kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.