Na Saidina Msangi, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yusuff Masauni ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuongeza kasi ya ukaguzi wa masuala ya ununuzi katika taasisi za Umma ili kubaini mapungufu na kuchukua hatua kabla ya kuisababishia Serikali hasara.

Mheshimiwa Masauni ametoa maagizo hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo akiwa katika ziara yake ya kutembelea Taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema kuwa Serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye ununuzi akitolea mfano Bajeti iliyopita ya Mwaka wa Fedha 2020/2021 ambapo Shilingi trilioni 25 sawa na asilimia 75 ya Bajeti yote zilitengwa kwa ajili ya kufanya ununuzi.

“Ili kudhibiti matumizi yasiyofaa ya fedha za Umma, ni lazima Idara ya ufuatiliaji na Ukidhi ipatiwe wafanyakazi wa kutosha na wenye weledi ili ukaguzi ufanyike kwa ufanisi na kupunguza hasara kwa Taifa” alisema Mhe. Masauni.

Maelekezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Yusuff Masauni yanakuja baada ya kuelezwa kuwa kutokana na changamoto ya uhaba wa watumishi katika Idara ya Ufuatiliaji na Ukidhi, PPRA inakagua wastani wa taasisi 120 katika taasisi 540 kwa mwaka.

Aidha, Dkt. Masauni aliipongeza Taasisi hiyo kwa kusimamia Mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Mtandao ujulikanao kama TaNEPS lakini akaagiza wataalam wa ndani wauboreshe ili kuhakikisha kuwa haitoi mwanya wa kutoa zabuni kwa watu wasio na vigezo na wanaotumia rushwa.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa mnapunguza uwezekano wa watumishi kukutana na wazabuni ana kwa ana ili kuepusha mazingira yanayoweza kuchochea rushwa na kuisababishia Serikali hasara” alisisitiza Mhe. Masauni.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi Serikalini (PPRA) Mhandisi Mary Swai, alisema kuwa Mamlaka yake inakabiliwa na upungufu wa watumishi ambapo kwa sasa ina watumishi 76 sawa na asilimia 48.

Alimshukuru Mhandisi Masauni kwa kuwatembelea kujua majukumu yao ya kila siku na kuahidi kuwa maagizo yote aliyowapatia yatafanyiwa kazi kikamilifu na kwamba wataendelea kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kuhakikisha kuwa sekta ya ununuzi wa umma inaleta tija na maslahi kwa Taifa.