Na. Hassan Mabuye, Pwani
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi aamuru kutiwa mbaroni matapeli watano maarufu wa kuuza na kunyanganya ardhi za watu Wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Waziri Lukuvi alitoa maagizo hayo jana wakati akiwa katika mkutano wa kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wakazi wa mkoa wa Pwani na kuzitolea ufumbuzi eneo la Mapinga Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Katika mkutano huo ambao wakazi wa eneo hilo walijitokeza na kutoa ushuhuda wa kutapeliwa maeneo yao kwa muda mrefu Waziri Lukuvi aliagiza kukamatwa kwa watu watano waliothibitika kutapeli viwanja na mashamba ya watu wengi akiwemo Katibu Muenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mapinga Wilaya ya Bagamoyo kufanyiwa mahojiano kwa tuhuma za kuhusika na utapeli wa kuuza maeneo na kusababisha migogoro katika kata hiyo.

Watuhumiwa hao ni Omari Shabani ambaye ni Katibu Muenezi wa kata ya Mapinga, Ramadhani Rashidi aliyekuwa katibu wa kitongoji cha Kiembeni, Marwa Muhoni, William Urio na Mwanahamis Habibu.

Mhe. Lukuvi alitoa amri kwa Kamanda wa Polisi wa wilaya ya Bagamoyo ya kuwaweka chini ya ulinzi watuhumiwa hao watano baada ya kutajwa na wananchi walioshiriki kwenye mkutano huo wakidaiwa kuhusika kuuza viwanja na mashamba kiholela na kusababisha migogoro ya ardhi ya kila mara.

“matapeli wengi wa ardhi hapa mkoa wa Pwani hasa Bagamoyo ni viongozi, viongozi wa mitaa na kata wanafanya utapeli, viongozi hata wa chama nimekuta kule viongozi wa mashina wanasaini nyaraka za mauziano ya ardhi. Kiongozi wa shina wa chama anahusikaje kuweka saini hati ya mauzino ya ardhi” alihoji Waziri Lukuvi.

Lukuvi alimuagiza mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo kufanya mahojiano ya kina na watuhumiwa hao na wakibainika hatua za kisheria zichukuliwe kukomesha migogoro ya ardhi.

Pamoja na wananchi kuwataja watuhumiwa hao pia Diwani wa kata ya Mapinga Chandika Dismas pamoja na baadhi ya viongozi walikiri kiongozi huyo wa Chama kuwa na jopo lake ambalo linashiriki kuuza maeneo na kuchochea migogoro katika eneo hilo.

Lukuvi ameitaja wilaya ya Bagamoyo hasa eneo la Mapinga kuongoza kwa migogoro ya ardhi ambayo imechangiwa na viongozi wa ngazi za chini wakiwemo viongozi wa mashina ya chama.

Lukuvi alisema migogoro hiyo imekua kero na kuwafanya wananchi kukosa amani na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.

“tayari ninayo majina ya watu 54 wanaodaiwa kuwa vinara wa kuuza ardhi katika Wilaya ya Bagamoyo wakiwemo Viongozi wa mitaa” Alisema Mhe. Likuvi.

Alionya baadhi ya viongozi wa chama cha Mapinduzi ( CCM) wanaojihusisha kuuza ardhi kwa kutumia mihuri ya Chama kuacha mara moja na hatua zitachukuliwa kwa atakayehusika.

Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi aliwataka wakazi wa Bagamoyo kuacha kuvamia maeneo ya Serikali ambayo hayajaendelezwa likiwemo la Lazaba linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema Viongozi wa Serikali wanatakiwa kulinda maeneo hayo pamoja na Lazaba yanayomilikiwa na Serikali kwani ipo mpango ya uwekezaji hivyo yeyote atakayevamia asitarajie kulipwa fidia.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge aliahidi kufanyia kazi malekezo ya Waziri kukomesha uvamizi wa Mkoa huo.

Kunenge alisema migogoro mingi katika Wilaya hiyo inadaiwa kuchangiwa na watendaji na Viongozi wa kisiasa.

Kaimu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo Abubakari Mlawa alikiri kupata taarifa za tuhuma za Viongozi hao na kusema "Kama chama tuhuma zilitufikia na taratibu za kufuatilia tuhuma hizo zinaendelea"

Alisema wanatarajia kukaa vikao na kujadili tuhuma za Viongozi hao na kwamba atakayebainika atavuliwa nafasi ya uongozi kwani Kata hiyo imekua kinara wa migogoro ya ardhi.

Mlawa ameongeza kuwa hatua hizo si kwa Viongozi wa chama tu hata Viongozi wa Serikali waliopata dhamana za uongozi wao kupitia chama Cha Mapinduzi ambao wametuhumiwa nao watachukuliwa hatua kali.