Kimbunga cha In-Fa kimepiga maeneo kadhaa ya mashariki mwa China na kusababisha mafuriko, japo hakukuwepo na ripoti za uharibifu mkubwa.
Kwa mujibu wa idara ya hali ya hewa ya China, usafiri wa anga na treni umesimamishwa katika eneo la pwani kwenye bandari muhimu ya usafirishaji wa mizigo ya Ningbo, sehemu ambako kimbunga kilipiga leo mchana.
Kimbunga hicho kimepiga wakati shughuli za uokoaji zikiendelea katika mkoa wa Henan ulioathirika na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua.
Maafisa wa serikali wamesema leo Jumapili kuwa watu wengine watano wamefariki kutokana na mafuriko katika mkoa wa Henan, na kuongeza idadi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko hayo imefikia 63.